Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 51:1-19

Zaburi 51:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Nihurumie, Ee Mungu, kadiri ya fadhili zako; ufutilie mbali makosa yangu, kadiri ya wingi wa huruma yako. Unioshe kabisa hatia yangu; unisafishe dhambi yangu. Nakiri kabisa makosa yangu, daima naiona waziwazi dhambi yangu. Nimekukosea wewe peke yako, nimetenda yaliyo mabaya mbele yako. Uamuzi wako ni wa haki hukumu yako haina lawama. Mimi ni mkosefu tangu kuzaliwa kwangu, mwenye dhambi tangu tumboni mwa mama yangu. Wewe wataka unyofu wa ndani; hivyo nifundishe hekima moyoni. Unitakase kwa husopo, nitakate; unioshe niwe mweupe pe. Nijaze furaha na shangwe, nifurahishe tena, mimi ambaye uliniponda. Ugeuke, usiziangalie dhambi zangu; uzifute hatia zangu zote. Uniumbie moyo safi, ee Mungu, uweke ndani yangu roho mpya na thabiti. Usinitupe mbali nawe; usiniondolee roho yako takatifu. Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa, utegemeze ndani yangu moyo wa utii. Hapo nitawafunza wakosefu njia yako, nao wenye dhambi watarudi kwako. Uniokoe na hatia ya umwagaji damu, ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, nami nitaimba kwa sauti kuwa umeniokoa. Uniwezeshe kusema, ee Bwana, midomo yangu itangaze sifa zako. Kwa kweli wewe hupendezwi na tambiko, ama sivyo mimi ningalikutolea. Wewe huna haja na tambiko za kuteketezwa. tambiko yangu kwako ee Mungu, ni moyo mnyofu; wewe, ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu. Ee Mungu, upende kuutendea mema mji wa Siyoni; uzijenge tena upya kuta za mji wa Yerusalemu. Hapo utapendezwa na tambiko za kweli: Sadaka za kuteketezwa na za kuteketezwa nzima; mafahali watatolewa tambiko madhabahuni pako.

Shirikisha
Soma Zaburi 51

Zaburi 51:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ee Mungu, unirehemu, kulingana na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu iko mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu. Tazama, nikazaliwa nikiwa na hatia; Mama yangu akanichukua mimba nikiwa na dhambi. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanifundisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya na kuithibiti roho yangu. Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya upendo. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na umwagaji wa damu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. Maana hupendezwi na dhabihu, na kama ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu. Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako.

Shirikisha
Soma Zaburi 51

Zaburi 51:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu. Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu. Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng’ombe Juu ya madhabahu yako.

Shirikisha
Soma Zaburi 51

Zaburi 51:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu. Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu. Kwa maana ninajua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima. Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako, ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo, na kuwa na haki utoapo hukumu. Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima. Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. Unipe kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda na ifurahi. Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu. Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu. Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze. Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watakugeukia wewe. Ee Mungu, Mungu uniokoaye, niokoe na hatia ya kumwaga damu, nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako. Ee BWANA, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako. Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta, hufurahii sadaka za kuteketezwa. Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau. Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi, ukazijenge upya kuta za Yerusalemu. Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki, sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana, pia mafahali watatolewa madhabahuni mwako.

Shirikisha
Soma Zaburi 51

Zaburi 51:1-19

Zaburi 51:1-19 BHNZaburi 51:1-19 BHNZaburi 51:1-19 BHNZaburi 51:1-19 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima