Zaburi 34:1-10
Zaburi 34:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Nitamtukuza Mwenyezi-Mungu nyakati zote, sitaacha kamwe kuzitamka sifa zake. Mimi nitaona fahari juu ya Mwenyezi-Mungu, wanyonge wasikie na kufurahi. Mtukuzeni Mwenyezi-Mungu pamoja nami, sote pamoja tulisifu jina lake. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu naye akanijibu, na kuniondoa katika hofu zangu zote. Mgeukieni Mungu mpate kufurahi; nanyi hamtaaibishwa kamwe. Maskini alimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamsikia, na kumwokoa katika taabu zake zote. Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao, na kuwaokoa katika hatari. Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema. Heri mtu anayekimbilia usalama kwake. Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake; maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu. Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa; lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema.
Zaburi 34:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nitamhimidi BWANA kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika BWANA nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie na kufurahi. Mtukuzeni BWANA pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nilimtafuta BWANA, naye akanijibu, Akaniokoa kutoka kwa hofu zangu zote. Mwelekezeeni macho, mpate kufurahi, Na nyuso zenu hazitaaibishwa kamwe. Maskini huyu aliita, BWANA akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa BWANA huwazungukia, Wamchao na kuwaokoa. Onjeni muone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumainia. Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Maana, wamchao hawapungukiwi kitu. Wanasimba hutindikiwa, na kuona njaa; Bali wamtafutao BWANA hawapungukiwi kitu chochote kilicho chema.
Zaburi 34:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nitamhimidi BWANA kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika BWANA nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mtukuzeni BWANA pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nalimtafuta BWANA akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya. Maskini huyu aliita, BWANA akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao BWANA hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
Zaburi 34:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nitamtukuza BWANA nyakati zote, sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote. Nafsi yangu itajisifu katika BWANA, walioonewa watasikia na wafurahi. Mtukuzeni BWANA pamoja nami, naam, na tulitukuze jina lake pamoja. Nilimtafuta BWANA naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote. Wale wamtazamao hutiwa nuru, nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe. Maskini huyu alimwita BWANA, naye akamsikia, akamwokoa katika taabu zake zote. Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa. Onjeni mwone kwamba BWANA ni mwema, heri mtu yule anayemkimbilia. Mcheni BWANA enyi watakatifu wake, kwa maana wale wamchao hawapungukiwi na chochote. Wana simba wenye nguvu hutindikiwa na kuona njaa, bali wale wamtafutao BWANA hawatakosa kitu chochote kilicho chema.