Zaburi 33:10-22
Zaburi 33:10-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa. Lakini mipango ya BWANA inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake. Kutoka mbinguni BWANA hutazama chini na kuwaona wanadamu wote; kutoka maskani mwake huwaangalia wote wakaao duniani: yeye ambaye huumba mioyo yao wote, ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda. Hakuna mfalme aokokaye kwa ukubwa wa jeshi lake; hakuna shujaa aokokaye kwa wingi wa nguvu zake. Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu, licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa. Lakini macho ya BWANA yako kwa wale wamchao, kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo, ili awaokoe na mauti, na kuwahifadhi wakati wa njaa. Sisi tunamngojea BWANA kwa matumaini, yeye ni msaada wetu na ngao yetu. Mioyo yetu humshangilia, kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu. Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee BWANA, tunapoliweka tumaini letu kwako.
Zaburi 33:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu hupangua mipango ya mataifa, na kuyatangua mawazo yao. Mpango wa Mwenyezi-Mungu hudumu milele; maazimio yake yadumu vizazi vyote. Heri taifa ambalo Mungu wake ni Mwenyezi-Mungu; heri wale aliowachagua kuwa watu wake mwenyewe! Mwenyezi-Mungu huangalia chini kutoka mbinguni, na kuwaona wanadamu wote. Kutoka kwenye kiti chake cha enzi, huwaangalia wakazi wote wa dunia. Yeye huunda mioyo ya watu wote, yeye ajua kila kitu wanachofanya. Mfalme hawezi kuokolewa kwa kuwa na jeshi kubwa; wala shujaa hapati ushindi kwa nguvu zake kubwa. Farasi wa vita hafai kitu kwa kupata ushindi; nguvu zake nyingi haziwezi kumwokoa mtu. Mwenyezi-Mungu huwaangalia wale wamchao, watu ambao wanatumainia fadhili zake. Yeye huwaokoa katika kifo, huwaweka hai wakati wa njaa. Mioyo yetu yamtumainia Mwenyezi-Mungu. Yeye ni msaada wetu na ngao yetu. Naam twafurahi kwa sababu yake; tuna matumaini katika jina lake takatifu. Fadhili zako zikae nasi, ee Mwenyezi-Mungu, kwani sisi tumekuwekea tumaini letu.
Zaburi 33:10-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huitangua mipango ya watu. Shauri la BWANA lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake. Toka mbinguni BWANA huchungulia, Huangalia na kuwaona wanadamu wote. Akiwa katika kiti chake cha enzi. Huwaangalia wote wakaao duniani. Yeye aiumbaye mioyo yao wote Na kuziona kazi zao zote. Mfalme haokolewi kwa jeshi lake kubwa, Wala shujaa haokoki kwa kuwa na nguvu nyingi. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. Ili kuwaponya nafsi zao kutoka kwa mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja BWANA; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu. Ee BWANA, fadhili zako zikae nasi, Kama tunavyo kutumainia Wewe.
Zaburi 33:10-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA huyabatilisha mashauri ya mataifa, Huyatangua makusudi ya watu. Shauri la BWANA lasimama milele, Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. Heri taifa ambalo BWANA ni Mungu wao, Watu aliowachagua kuwa urithi wake. Toka mbinguni BWANA huchungulia, Huwatazama wanadamu wote pia. Toka mahali pake aketipo Huwaangalia wote wakaao duniani. yeye aiumbaye mioyo yao wote Huzifikiri kazi zao zote. Hapana mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja BWANA; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu. Ee BWANA, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.