Zaburi 144:1-15
Zaburi 144:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu, anayeipa mikono yangu mazoezi ya vita, na kuvifunza vidole vyangu kupigana. Yeye ni rafiki yangu amini na ngome yangu, kinga yangu na mkombozi wangu; yeye ni ngao yangu, kwake napata usalama; huyashinda mataifa na kuyaweka chini yangu. Ee Mwenyezi-Mungu, mtu ni nini hata umjali? Mwanadamu ni nini hata umfikirie? Binadamu ni kama pumzi tu; siku zake ni kama kivuli kipitacho. Uinamishe mbingu zako, ee Mwenyezi-Mungu, ushuke chini! Uiguse milima nayo itoe moshi! Lipusha umeme, uwatawanye maadui; upige mishale yako, uwakimbize! Unyoshe mkono wako kutoka juu, uniokoe na kuniondoa katika maji haya mengi; uniondoe makuchani mwa wageni, ambao husema maneno ya uongo, hunyosha mkono kushuhudia uongo. Nitakuimbia wimbo mpya, ee Mungu; nitakupigia kinubi cha nyuzi kumi, wewe uwapaye wafalme ushindi, umwokoaye Daudi mtumishi wako! Uniokoe na upanga wa adui katili, uniondoe makuchani mwa wageni, ambao husema maneno ya uongo, hunyosha mkono kushuhudia uongo. Wavulana wetu wakue kikamilifu kama mimea bustanini; binti zetu wawe kama nguzo zilizochongwa kupambia ikulu. Ghala zetu zijae mazao ya kila aina. Kondoo wetu mashambani wazae maelfu kwa maelfu. Mifugo yetu iwe na afya na nguvu; isitupe mimba wala kuzaa kabla ya wakati. Kusiwepo tena udhalimu mitaani mwetu. Heri taifa ambalo limejaliwa hayo! Heri taifa ambalo Mungu wao ni Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 144:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na ahimidiwe BWANA, mwamba wangu, Aifundishaye mikono yangu vita, Na vidole vyangu kupigana. Mwamba wangu na ngome yangu, Nguzo yangu na mwokozi wangu Ngao yangu ninayemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu. Ee BWANA, mtu ni kitu gani hata umjali? Na binadamu hata umwangalie? Binadamu ni kama ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho. Ee BWANA, uziinamishe mbingu zako, ushuke chini. Uiguse milima ili nayo itoe moshi. Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe. Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, kutoka kwa mkono wa wageni, Vinywa vyao vinasema visivyofaa, Na ambao mikono yao ya kulia ni ya uongo. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia. Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kulia ni mkono wa uongo. Wavulana wetu wakiwa ujanani wawe kama miche Iliyostawi kikamilifu. Binti zetu wawe kama nguzo za pembeni Zilizochongwa ili kupamba kasri. Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu. Ng'ombe wetu na wabebe mizigo mizito, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu. Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye BWANA kuwa Mungu wao.
Zaburi 144:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na ahimidiwe BWANA, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana. Mhisani wangu na boma langu, Ngome yangu na mwokozi wangu, Ngao yangu niliyemkimbilia, Huwatiisha watu wangu chini yangu. Ee BWANA, mtu ni kitu gani hata umjue? Na binadamu hata umwangalie? Binadamu amefanana na ubatili, Siku zake ni kama kivuli kipitacho. BWANA, uziinamishe mbingu zako, ushuke, Uiguse milima nayo itatoka moshi. Utupe umeme, uwatawanye, Uipige mishale yako, uwafadhaishe. Uinyoshe mikono yako toka juu, uniponye, Unitoe katika maji mengi, katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia. Awapaye wafalme wokovu, Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. Uniponye, unitoe, Katika mkono wa wageni. Vinywa vyao vyasema visivyofaa, Na mkono wao wa kuume ni mkono wa uongo. Wana wetu na wawe kama miche Waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni Zilizonakishwa kwa kupamba hekalu. Ghala zetu na zijae Zenye akiba za jinsi zote. Kondoo zetu na wazae Elfu na makumi elfu mashambani mwetu. Ng’ombe zetu na wachukue mizigo, Kusiwe na kushambuliwa. Wala kusiwe na kuhamishwa, Wala malalamiko katika njia zetu. Heri watu wenye hali hiyo, Heri watu wenye BWANA kuwa Mungu wao.
Zaburi 144:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sifa ni kwa BWANA Mwamba wangu, aifundishaye mikono yangu vita, na vidole vyangu kupigana. Yeye ni Mungu wangu wa upendo na boma langu, ngome yangu na mwokozi wangu, ngao yangu ninayemkimbilia, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu. Ee BWANA, mwanadamu ni nini hata umjali, Binadamu ni nini hata umfikirie? Mwanadamu ni kama pumzi, siku zake ni kama kivuli kinachopita. Ee BWANA, pasua mbingu zako, ushuke, gusa milima ili itoe moshi. Peleka umeme uwatawanye adui, lenga mishale yako uwashinde. Nyoosha mkono wako kutoka juu, nikomboe na kuniokoa kutoka maji makuu, kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia, kwa Yule awapaye wafalme ushindi, ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake kutokana na upanga hatari. Nikomboe na uniokoe kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. Kisha wana wetu wakati wa ujana wao watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa kurembesha jumba la kifalme. Ghala zetu zitajazwa aina zote za mahitaji. Kondoo zetu watazaa kwa maelfu, kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu; maksai wetu watakokota mizigo mizito. Hakutakuwa na kubomoka kuta, hakuna kuchukuliwa mateka, wala kilio cha taabu katika barabara zetu. Heri watu ambao hili ni kweli; heri wale ambao BWANA ni Mungu wao.