Methali 4:14-27
Methali 4:14-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Usijiingize katika njia ya waovu, wala usifuate mwenendo wa watu wabaya. Iepe njia hiyo wala usiikaribie; jiepushe nayo, uende zako. Waovu kamwe hawalali wasipotenda uovu; hawapati usingizi wasipomkwaza mtu. Maana uovu ndicho chakula chao, ukatili ndiyo divai yao. Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, sikiliza kwa makini maneno yangu, itegee sikio misemo yangu. Usiyaache yatoweke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako. Maana hayo ni uhai kwa mtu anayeyapata, ni dawa kwa mwili wake wote. Linda moyo wako kwa uangalifu wote, maana humo zatoka chemchemi za uhai. Tenga mbali nawe lugha potovu; wala midomo yako isitamke maneno madanganyifu. Uyaelekeze macho yako mbele kwa ujasiri, mtazamo wako uwe mbele moja kwa moja. Fikiria njia utakayochukua, na hatua zako zote zitakuwa kamili. Usigeukie kulia wala kushoto; epusha mguu wako mbali na uovu.
Methali 4:14-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya ujeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Jiepushe na kinywa cha ujeuri, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kulia wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.
Methali 4:14-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, Ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe. Macho yako yatazame mbele, Na kope zako zitazame mbele yako sawasawa. Ulisawazishe pito la mguu wako, Na njia zako zote zithibitike; Usigeuke kwa kuume wala kwa kushoto; Ondoa mguu wako maovuni.
Methali 4:14-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu, wala usitembee katika njia ya wapotovu. Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako. Kwa kuwa hawawezi kulala hadi watende uovu; wanashindwa hata kusinzia hadi wamwangushe mtu. Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri. Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hung’aa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako; kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu. Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako. Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako. Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika. Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.