Hesabu 9:15-23
Hesabu 9:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ambayo hema takatifu lilisimikwa, wingu lilishuka na kulifunika hema la maamuzi. Wakati wa usiku wingu hilo lilionekana kama moto mpaka asubuhi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kila siku; wingu lililifunika hema mchana, na usiku lilionekana kama moto. Kila mara wingu hilo lilipoinuliwa juu ya hema, Waisraeli walivunja kambi na kupiga kambi tena mahali wingu hilo lilipotua. Walisafiri kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, na kupiga kambi tena kwa amri yake. Muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, watu walikaa katika kambi hiyo. Hata kama wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku nyingi, Waisraeli walimtii Mwenyezi-Mungu, nao hawakuondoka. Wakati mwingine wingu hilo lilikaa juu ya hema kwa muda wa siku chache tu; lakini kila wakati Waisraeli walibaki kambini; walihama kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Wakati mwingine wingu lilikaa juu ya hema tangu jioni mpaka asubuhi tu; na mara tu lilipoinuliwa, hao watu pia walifunga safari. Na ikiwa lilikaa juu ya hema mchana kutwa na usiku kucha, wao waliondoka tu wingu lilipoinuliwa. Ikiwa ni siku mbili, mwezi, mwaka au zaidi, muda wote wingu hilo lilipokuwa juu ya hema, Waisraeli hawakuhama; lakini lilipoinuliwa, nao pia walihama. Kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walipiga kambi na kwa agizo la Mwenyezi-Mungu walisafiri. Walishika agizo la Mwenyezi-Mungu kama alivyotoa amri yake kwa njia ya Mose.
Hesabu 9:15-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi. Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku. Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao. Kwa amri ya BWANA Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya BWANA walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao. Hata lile wingu lilipokawia juu ya maskani siku nyingi, wana wa Israeli walimtii BWANA, na hawakusafiri. Na pengine lile wingu lilikaa juu ya maskani siku chache; ndipo kwa amri ya BWANA walikaa katika kambi yao, tena kwa amri ya BWANA walisafiri. Na pengine lile wingu lilikaa tangu jioni hata asubuhi; na lile wingu lilipoinuliwa asubuhi walisafiri, au kama likikaa usiku na mchana pia, lilipoinuliwa lile wingu, ndipo waliposafiri. Ikiwa lile wingu lilikawia, likikaa juu ya maskani siku mbili, au mwezi, au mwaka, wana wa Israeli walikaa katika kambi yao, wasisafiri; bali lilipoinuliwa walisafiri. Kwa amri ya BWANA walipiga kambi yao, na kwa amri ya BWANA walisafiri; walimtii BWANA, kwa mkono wa Musa.
Hesabu 9:15-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi. Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku. Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao. Kwa amri ya BWANA Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya BWANA walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao. Na lile wingu lilipokawia juu ya maskani siku nyingi, ndipo wana wa Israeli walipolinda malinzi ya BWANA, wala hawakusafiri. Na pengine lile wingu lilikaa juu ya maskani siku chache; ndipo kwa amri ya BWANA walikaa katika kambi yao, tena kwa amri ya BWANA walisafiri. Na pengine lile wingu lilikaa tangu jioni hata asubuhi; na lile wingu lilipoinuliwa asubuhi walisafiri, au kama likikaa usiku na mchana pia, lilipoinuliwa lile wingu, ndipo waliposafiri. Ikiwa lile wingu lilikawia, likikaa juu ya maskani siku mbili, au mwezi, au mwaka, wana wa Israeli walikaa katika kambi yao, wasisafiri; bali lilipoinuliwa walisafiri. Kwa amri ya BWANA walipiga kambi yao, na kwa amri ya BWANA walisafiri; wakayalinda malinzi ya BWANA, kwa mkono wa Musa.
Hesabu 9:15-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku hiyo ambayo Maskani, Hema la Ushuhuda, iliposimamishwa, wingu liliifunika. Kuanzia jioni mpaka asubuhi wingu lililokuwa juu ya Maskani lilionekana kama moto. Hivyo ndivyo lilivyoendelea kuwa; wingu liliifunika wakati wa mchana, na usiku lilionekana kama moto. Wakati wowote wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, nao Waisraeli waliondoka; mahali popote wingu liliposimama, Waisraeli walipiga kambi. Kwa amri ya BWANA Waisraeli waliondoka, na kwa amri yake walipiga kambi. Kwa muda wote wingu liliposimama juu ya Maskani, Waisraeli walibaki wamepiga kambi. Wakati wingu lilipobaki juu ya Maskani kwa muda mrefu, Waisraeli walitii amri ya BWANA nao hawakuondoka. Wakati mwingine wingu lilikuwa juu ya Maskani kwa siku chache tu; kwa amri ya BWANA wangelipiga kambi na kisha kwa amri yake wangeliondoka. Wakati mwingine wingu lilikuwepo kuanzia jioni mpaka asubuhi tu, na lilipoinuka asubuhi, nao waliondoka. Ikiwa ni mchana au usiku, wakati wowote wingu lilipoinuka, waliondoka. Ikiwa wingu lilikaa juu ya Maskani kwa siku mbili au mwezi au mwaka, Waisraeli wangebaki wamepiga kambi na hawakuondoka; lakini lilipoinuka, wangeondoka. Kwa amri ya BWANA walipiga kambi, na kwa amri ya BWANA waliondoka. Walitii amri ya BWANA, kufuatana na agizo lake kupitia Mose.