Hesabu 10:29-36
Hesabu 10:29-36 Biblia Habari Njema (BHN)
Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.” Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.” Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu. Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.” Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi. Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana. Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.” Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.”
Hesabu 10:29-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopiga kambi, nawe utakuwa kiongozi wetu. Isitoshe, ukienda pamoja nasi, naam, mema yote ambayo BWANA atatutendea, nawe tutakutendea vivyo hivyo. Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la Agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.
Hesabu 10:29-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho. Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote BWANA atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo. Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.
Hesabu 10:29-36 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Mose akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Mose, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo BWANA amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja nasi tutakutendea mema, kwa maana BWANA ameahidi mambo mema kwa Israeli.” Akajibu, “Hapana, sitakwenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.” Lakini Mose akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali ambapo yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu. Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na BWANA.” Hivyo waliondoka kutoka mlima wa BWANA, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la BWANA liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Wingu la BWANA lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini. Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Mose alisema, “Ee BWANA, inuka! Watesi wako na watawanyike; adui zako na wakimbie mbele zako.” Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema, “Ee BWANA, rudi, kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”