Nehemia 1:4-11
Nehemia 1:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni. Kisha nikasema: “Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wampendao na kutii amri zake, tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako. Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Mose mtumishi wako. “Kumbuka agizo ulilompa Mose mtumishi wako, ukisema, ‘Kama mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa, lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni wako mbali sana katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali ambapo nimepachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’ “Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu. Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.” Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.
Nehemia 1:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni, nikisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbinguni, wewe u Mungu aliye mkuu na wa kutisha, unalishika agano lako na unawafadhili wale wakupendao na kuzishika amri zako. Yasikilize kwa makini maombi yangu, na uniangalie mimi mtumishi wako, ninapokuomba kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli, usiku na mchana. Ninaungama dhambi za watu wa Israeli, tulizofanya mbele yako. Mimi pamoja na watu wa jamaa yangu tumefanya dhambi. Tumetenda mabaya mbele yako, hatujazishika amri zako, kanuni na maagizo yako uliyomwagiza mtumishi wako Mose. Kumbuka sasa lile ulilomwambia mtumishi wako Mose, uliposema, ‘Kama hamtakuwa waaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa. Lakini mkinirudia, mkazishika amri zangu na kuzifuata hata ingawa nitakuwa nimewatawanya mbali kabisa, nitawarudisha mahali nilipochagua kuwa mahali pangu pa kuabudiwa.’ Watu wa Israeli ni watumishi wako na watu wako uliwakomboa kwa uwezo wako na mkono wako wenye nguvu. Ee Bwana, yasikie maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watumishi wako wanaofurahia kukutii wewe. Nakuomba unifanikishe leo, mimi mtumishi wako, na kunijalia kuhurumiwa na mfalme.” Basi, mimi nilikuwa na jukumu la kumpa mfalme kinywaji.
Nehemia 1:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadhaa; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni; nikasema, Nakusihi, Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake; tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi. Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako. Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa; bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo. Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari. Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nilikuwa mnyweshaji wa mfalme).
Nehemia 1:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni; nikasema, Nakusihi, Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake; tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi. Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako. Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa; bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo. Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari. Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme).