Marko 16:11-20
Marko 16:11-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini hao waliposikia kwamba yu hai, naye amemwona, hawakuamini. Baada ya hayo akawatokea wawili miongoni mwao, akiwa na sura nyingine; nao walikuwa wakitembea njiani kwenda mashambani. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwaamini. Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutoamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kulia wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]
Marko 16:11-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki. Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia. Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka. Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.” Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]
Marko 16:11-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini waliposikia ya kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria Magdalene amemwona, hawakuamini. Baadaye Yesu aliwatokea wanafunzi wawili akiwa na sura nyingine. Wanafunzi hao walikuwa wanakwenda shambani. Nao pia wakaenda, wakawaambia wenzao. Hata hivyo hawakuamini. Mwishowe Yesu aliwatokea wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa pamoja mezani. Akawakemea sana kwa sababu ya kutoamini kwao na ukaidi wao, maana hawakuwaamini wale waliokuwa wamemwona baada ya kufufuka. Basi, akawaambia, “Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu. Anayeamini na kubatizwa ataokolewa. Asiyeamini atahukumiwa. Na ishara hizi zitaandamana na wale wanaoamini: Kwa jina langu watatoa pepo na watasema kwa lugha mpya. Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawawekea wagonjwa mikono, nao watapona.” Basi, Bwana Yesu alipokwisha sema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi upande wa kulia wa Mungu. Wanafunzi wakaenda wakihubiri kila mahali. Bwana akafanya kazi pamoja nao na kuimarisha ujumbe huo kwa ishara zilizoandamana nao.]
Marko 16:11-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki. Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki. Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]