Marko 16:11-20
Marko 16:11-20 SRUV
Lakini hao waliposikia kwamba yu hai, naye amemwona, hawakuamini. Baada ya hayo akawatokea wawili miongoni mwao, akiwa na sura nyingine; nao walikuwa wakitembea njiani kwenda mashambani. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwaamini. Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutoamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Nendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kulia wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]