Marko 15:21-32
Marko 15:21-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipokuwa njiani, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni, mwenyeji wa Kurene. Yeye alikuwa baba yao Aleksanda na Rufo, na wakati huo alikuwa akitoka shambani. Basi, wakamlazimisha achukue msalaba wa Yesu. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa. Wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini yeye alikataa kunywa. Basi, wakamsulubisha, wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura waamue nani angepata nini. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. Na shtaka dhidi yake lilikuwa limeandikwa, “Mfalme wa Wayahudi.” Pamoja naye waliwasulubisha wanyanganyi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. [ Hapo yakatimia Maandiko Matakatifu yanayosema, “Aliwekwa kundi moja na waovu.”] Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana, wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe mwenye kuvunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu! Sasa, shuka msalabani ujiokoe mwenyewe!” Nao makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni Kristo, Mfalme wa Israeli! Basi, na ashuke kutoka msalabani ili tuone na kuamini.” Hata watu wale waliosulubiwa pamoja naye walimtukana.
Marko 15:21-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashambani, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulubisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulubisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kulia na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulubiwa pamoja naye wakamsuta.
Marko 15:21-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulibisha wanyang’anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.
Marko 15:21-32 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anaingia mjini kutoka mashambani, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. Kisha wakampeleka Isa hadi mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua. Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: MFALME WA WAYAHUDI. Pamoja naye walisulubiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ Nalo andiko likatimizwa, lisemalo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”] Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!” Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa Torati wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Basi huyu Al-Masihi, huyu mfalme wa Israeli, ashuke sasa msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.