Marko 15:21-32
Marko 15:21-32 SRUV
Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashambani, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulubisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulubisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulubisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kulia na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulubiwa pamoja naye wakamsuta.