Mathayo 10:1-23
Mathayo 10:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote. Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: Wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu. Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. “Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi. Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora. “Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa. Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. “Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa. “Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.
Mathayo 10:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskarioti, naye ndiye aliyemsaliti. Hao Kumi na Wawili Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Bali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala pesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mfanyakazi astahili posho yake. Na mji wowote au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hadi mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule. Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwaua. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.
Mathayo 10:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule. Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.
Mathayo 10:1-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndipo Isa akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina. Haya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili: wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Isa. Hawa kumi na wawili, Isa aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. Mnapoenda, hubirini ujumbe huu, ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu. Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake. “Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake hadi mtakapoondoka. Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung’uteni mavumbi kutoka miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo. “Tazama ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa-mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua. “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao. Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa. Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu. “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.