Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 10:1-23

Mathayo 10:1-23 SRUV

Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskarioti, naye ndiye aliyemsaliti. Hao Kumi na Wawili Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Bali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala pesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mfanyakazi astahili posho yake. Na mji wowote au kijiji chochote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hadi mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule. Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwaua. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

Soma Mathayo 10