Luka 7:1-10
Luka 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kusema yale aliyotaka watu wasikie, Yesu alikwenda Kafarnaumu. Huko kulikuwa na jemadari mmoja ambaye alikuwa na mtumishi wake aliyempenda sana. Huyu mtumishi alikuwa mgonjwa karibu na kufa. Yule jemadari aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee fulani Wayahudi waende kumwomba aje kumponya mtumishi wake. Walipofika kwa Yesu, walimsihi sana, wakasema: “Huyu anastahili afanyiwe jambo hilo, kwa maana yeye analipenda taifa letu, na ndiye aliyetujengea lile sunagogi.” Basi, Yesu akaenda pamoja nao. Alipokuwa karibu na kufika nyumbani kwa yule jemadari, yule jemadari aliwatuma marafiki zake wamwambie Yesu: “Bwana, usijisumbue zaidi, maana mimi sistahili uingie nyumbani mwangu. Ndio maana sikujiona nastahili hata kuja kwako. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi pia ni mtu niliye chini ya mamlaka, na ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; namwambia mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” Yesu aliposikia hayo, alishangaa, halafu akauelekea ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akasema, “Sijaona mwenye imani kama hii hata katika Israeli!” Wale watu walipowasili nyumbani walimkuta yule mtumishi hajambo kabisa.
Luka 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake afisa mmoja alikuwa mgonjwa, karibu kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule afisa alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari langu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.
Luka 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.
Luka 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu. Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu kufa. Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari. Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili, kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.” Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Ndiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.