Luka 7:1-10
Luka 7:1-10 NEN
Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu. Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu kufa. Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari. Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili, kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.” Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Ndiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.” Yesu aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.