Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 3:1-23

Luka 3:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mtawala wa Galilaya, na ndugu yake Filipo alikuwa mtawala wa eneo la Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mtawala wa Abilene, na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane mwana wa Zakaria, kule jangwani. Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani. Akawa anahubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi. Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni barabara zake. Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyoshwa, njia mbaya zitatengenezwa. Na, watu wote watauona wokovu aletao Mungu.’” Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea muikimbie ghadhabu inayokuja? Onesheni kwa vitendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kujisemea: ‘Baba yetu ni Abrahamu!’ Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu. Basi, shoka liko tayari kwenye mizizi ya miti; hivyo kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.” Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?” Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.” Nao watozaushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?” Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.” Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.” Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane, kuwa labda yeye ndiye Kristo. Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Yeye anacho mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka aipure nafaka yake, akusanye ngano katika ghala, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.” Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema. Lakini Yohane alimgombeza mtawala Herode, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya. Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani. Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka, na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.” Yesu alipoanza kazi yake hadharani alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mtoto wa Yosefu mwana wa Heli.

Shirikisha
Soma Luka 3

Luka 3:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa mtawala wa Yudea, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika katika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopindika patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa; Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu. Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazawa wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Abrahamu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Abrahamu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa kwenye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtosheke na mishahara yenu. Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza mioyoni mwao kuhusu Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza kamba ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye ungo wake uko mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanja wake wa kupuria, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiria watu. Lakini mfalme Herode alipokaripiwa na yeye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na maovu yote aliyoyafanya Herode, aliongeza na hili juu ya yote, alimfunga Yohana gerezani. Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa na umri wa miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli

Shirikisha
Soma Luka 3

Luka 3:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa; Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu. Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi? Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu. Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo, Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto; ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika. Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu. Lakini mfalme Herode alipokaripiwa na yeye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na maovu yote aliyoyafanya Herode, aliongeza na hili juu ya yote, alimfunga Yohana gerezani. Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe. Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli

Shirikisha
Soma Luka 3

Luka 3:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene, nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko jangwani. Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitashushwa. Njia zilizopinda zitanyooshwa, na zilizoparuza zitasawazishwa. Nao watu wote watauona wokovu wa Mungu.’ ” Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya. Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?” Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.” Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?” Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.” Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.” Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo. Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema. Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yohana gerezani. Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.” Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu

Shirikisha
Soma Luka 3