Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 3:1-23

Luka 3:1-23 NENO

Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Yudea, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene, nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yahya, mwana wa Zakaria huko jangwani. Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu, yanyoosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitashushwa. Njia zilizopinda zitanyooshwa, na zilizoparuza zitasawazishwa. Nao watu wote watauona wokovu wa Mungu.’” Yahya akaambia umati ule wa watu waliokuwa wanakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Ibrahimu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto kutoka mawe haya. Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” Umati ule wa watu wakamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?” Yahya akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.” Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Mwalimu na sisi inatupasa tufanyeje?” Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.” Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.” Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yahya angeweza kuwa ndiye Al-Masihi. Yahya akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho wa Mungu na kwa moto. Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.” Basi, kwa maonyo mengine mengi Yahya aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema. Lakini Yahya alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yahya gerezani. Baada ya watu wote kubatizwa, Isa naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. Roho Mtakatifu wa Mungu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.” Isa alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yusufu.