Luka 24:44-53
Luka 24:44-53 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu akawaambia, “Hii ndiyo maana ya maneno niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi: Kwamba ilikuwa lazima kukamilisha yote yaliyoandikwa juu yangu katika sheria ya Mose na katika vitabu vya manabii na katika kitabu cha Zaburi.” Kisha, akaziangazia akili zao ili wapate kuelewa Maandiko Matakatifu. Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu, na kwamba ni lazima, kwa jina lake, mataifa yote kuanzia Yerusalemu, yahubiriwe kwamba watu wanapaswa kutubu na kusamehewa dhambi. Nyinyi ni mashahidi wa mambo hayo. Nami mwenyewe nitawapelekeeni yule ambaye Baba aliahidi kumtuma, lakini ngojeni huku mjini mpaka mtakapopewa ile nguvu itokayo juu.” Kisha akawaongoza nje ya mji hadi Bethania, akainua mikono yake juu, akawabariki. Alipokuwa anawabariki, akawaacha; akachukuliwa mbinguni. Wao wakamwabudu, kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kubwa: Wakakaa muda wote hekaluni wakimsifu Mungu.
Luka 24:44-53 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika vitabu vya Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunua akili zao wapate kuelewa maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hadi mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kuu. Nao daima walikuwa ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.
Luka 24:44-53 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.
Luka 24:44-53 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.” Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. Ninyi ni mashahidi wa mambo haya. “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.” Akiisha kuwaongoza mpaka kwenye viunga vya Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki. Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni. Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.