Lk 24:44-53
Lk 24:44-53 SUV
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu. Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki. Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni. Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.