Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:26-56

Luka 23:26-56 Biblia Habari Njema (BHN)

Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: ‘Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!’ Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: ‘Tuangukieni!’ Na vilima, ‘Tufunikeni!’ Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?” Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!” Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.” Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.” Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo. Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.” Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamjibu, “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa, na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho. Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.” Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo. Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika. Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao. Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Kisha akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika. Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza. Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa. Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi ya kuupaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.

Shirikisha
Soma Luka 23

Luka 23:26-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shambani, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulubisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hadi saa tisa, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipigapiga vifua. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakatayarisha manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

Shirikisha
Soma Luka 23

Luka 23:26-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

Shirikisha
Soma Luka 23

Luka 23:26-56 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni Mkirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa. Idadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. Isa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao tumbo zao hazikuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ Ndipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!” ’ Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?” Watu wawili wahalifu walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe. Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walimsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume, na mwingine upande wake wa kushoto. Isa akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura. Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.” Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, na wakamwambia, “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.” Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo? Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.” Kisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika ufalme wako.” Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.” Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya. Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa raia wa Arimathaya huko Yudea, naye alikuwa anaungojea ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. Yusufu alienda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa. Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza. Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa. Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.

Shirikisha
Soma Luka 23