Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:26-56

Luka 23:26-56 NENO

Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni Mkirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Isa. Idadi kubwa ya watu wakamfuata Isa, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. Isa akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao tumbo zao hazikuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ Ndipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!” ’ Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?” Watu wawili wahalifu walipelekwa pamoja na Isa ili wakasulubiwe. Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walimsulubisha Isa pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume, na mwingine upande wake wa kushoto. Isa akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura. Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Al-Masihi wa Mungu, Mteule wake.” Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, na wakamwambia, “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Al-Masihi? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.” Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu hiyo hiyo? Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.” Kisha akasema, “Isa, unikumbuke utakapokuja katika ufalme wako.” Isa akamjibu, “Amin, nakuambia, leo utakuwa pamoja nami Paradiso.” Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa, kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili. Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho. Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.” Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao. Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya. Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa raia wa Arimathaya huko Yudea, naye alikuwa anaungojea ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa. Yusufu alienda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa. Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado. Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza. Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa. Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.