Luka 23:1-22,24-25
Luka 23:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato. Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.” Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.” Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.” Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.” Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?” Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu. Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza. Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana. Basi, Herode pamoja na askari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato. Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki. Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu, akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake. Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo. Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.” [ Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.] Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!” ( Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.) Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena; lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!” Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya ubaya gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
Luka 23:24-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe. Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa kusababisha uasi na mauaji; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
Luka 23:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha mkutano wote wakasimama, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na mkutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. Nao walisisitiza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Yudea yote, tokea Galilaya mpaka huku. Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akatarajia kuona ishara iliyofanywa na yeye. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lolote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamdhalilisha, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lolote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lolote alilolitenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulubishe. Msulubishe. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.
Luka 23:24-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.
Luka 23:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku. Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.
Lk 23:24-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.
Luka 23:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha umati wote wa watu ukainuka na kumpeleka Yesu kwa Pilato. Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Kristo, mfalme.” Basi Pilato akamuuliza Yesu, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe wasema.” Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwepo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!” Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!” Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?” Alipofahamu kwamba Yesu alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu. Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha. Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Yesu hakumjibu lolote. Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana. Herode na askari wake wakamdhihaki Yesu na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato. Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao. Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [ Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.] Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!” (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.) Pilato, akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena. Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”