Lk 23:1-22, 24-25
Lk 23:1-22 SUV
Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku. Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.
Lk 23:24-25 SUV
Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.