Luka 16:14-18
Luka 16:14-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu. Hapo akawaambia, “Nyinyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka. “Sheria na maandishi ya manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohane Mbatizaji. Tangu hapo, ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya sheria kufutwa. “Yeyote anayempa mkewe talaka na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.
Luka 16:14-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki. Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu. Torati na Manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo Habari Njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati. Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.
Luka 16:14-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki. Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu. Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu. Lakini ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati. Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.
Luka 16:14-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. Yesu akawaambia, “Ninyi mnajionyesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo. “Sheria na Manabii vilihubiriwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria. “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.