Luka 16:14-18
Luka 16:14-18 NEN
Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. Yesu akawaambia, “Ninyi mnajionyesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo. “Sheria na Manabii vilihubiriwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu. Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria. “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.