Luka 12:13-33
Luka 12:13-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mfano, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, lakini Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine? Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa katika tanuri, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba? Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msiwe na wasiwasi, kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo. Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwizi, wala nondo haharibu.
Luka 12:13-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.” Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?” Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” Kisha akawaambia mfano: “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’ Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada. “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
Luka 12:13-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine? Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba? Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi, kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo. Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.
Luka 12:13-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.” Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.” Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’ “Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika; kula, unywe, ufurahi.” ’ “Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’ “Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine? “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia. “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu.