Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 12:13-33

Luka 12:13-33 SRUV

Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu? Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mfano, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu. Akawaambia wanafunzi wake, Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, lakini Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine? Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa katika tanuri, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba? Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msiwe na wasiwasi, kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo. Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwizi, wala nondo haharibu.

Soma Luka 12