Luka 11:37-54
Luka 11:37-54 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika nyumbani mwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani. Yule Farisayo akashangaa kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula. Ndipo Bwana akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na uovu. Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye alitengeneza na ndani pia? Basi toeni sadaka ya vile mlivyo navyo, na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu. “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza. “Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kukalia viti vya mbele katika masinagogi, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. “Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.” Mtaalamu mmoja wa sheria akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.” Yesu akamjibu, “Nanyi wataalamu wa sheria, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia. “Ole wenu, kwa sababu ninyi mnajenga makaburi ya manabii waliouawa na baba zenu. Hivyo ninyi mwashuhudia na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya. Wao waliwaua manabii, nanyi mnawajengea makaburi. Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’ Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zekaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote. “Ole wenu ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.” Yesu alipoondoka huko, walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali, wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.
Luka 11:37-54 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipokuwa akiongea, Mfarisayo mmoja alimkaribisha chakula nyumbani kwake, naye akaenda, akaketi kula chakula. Huyo Mfarisayo alistaajabu kuona kwamba alikula chakula bila kunawa kwanza. Bwana akamwambia, “Nyinyi Mafarisayo huosha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa udhalimu na uovu. Wapumbavu nyinyi! Je, aliyetengeneza nje si ndiye aliyetengeneza ndani pia? Toeni kwa maskini vile vitu vilivyomo ndani, na vingine vyote vitakuwa halali kwenu. “Lakini ole wenu Mafarisayo, kwa sababu mnatoza watu zaka hata juu ya majani ya kukolezea chakula, mchicha na majani mengine, na huku hamjali juu ya haki na upendo kwa Mungu. Mambo haya iliwapasa muwe mmeyazingatia bila kuyasahau yale mengine. “Ole wenu nyinyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kuketi mbele mahali pa heshima katika masunagogi, na kusalimiwa kwa heshima hadharani. Ole wenu, kwa sababu mko kama makaburi yaliyofichika; watu hutembea juu yake bila kufahamu.” Mmoja wa waalimu wa sheria akamwambia, “Mwalimu, maneno yako yanatukashifu na sisi pia.” Yesu akamjibu, “Na nyinyi waalimu wa sheria, ole wenu; maana mnawatwika watu mizigo isiyochukulika, huku nyinyi wenyewe hamnyoshi hata kidole kuwasaidia. Ole wenu, kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii wale ambao wazee wenu waliwaua. Kwa hiyo mnashuhudia na kukubaliana na matendo ya wazee wenu; maana wao waliwaua hao manabii, nanyi mnajenga makaburi yao. Kwa hiyo, Hekima ya Mungu ilisema hivi: ‘Nitawapelekea manabii na mitume, lakini watawaua baadhi yao, na kuwatesa wengine.’ Matokeo yake ni kwamba kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu ya damu ya manabii wote iliyomwagika tangu mwanzo wa ulimwengu; tangu kumwagwa damu ya Abeli mpaka ile ya Zekaria ambaye walimuua kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, hakika kizazi hiki kitaadhibiwa kwa matendo hayo. “Ole wenu nyinyi waalimu wa sheria, kwa sababu mmeuficha ule ufunguo wa mlango wa elimu; nyinyi wenyewe hamkuingia na mmewazuia waliokuwa wanaingia wasiingie.” Alipokuwa akitoka pale, wale Mafarisayo na waalimu wa sheria walianza kumshambulia vikali na kumsonga kwa maswali mengi ili wapate kumnasa kwa maneno yake.
Luka 11:37-54 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wanasheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, Waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.
Luka 11:37-54 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.