Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 11:37-54

Luka 11:37-54 SRUV

Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu. Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wanasheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, Waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.

Soma Luka 11