Maombolezo 4:12-22
Maombolezo 4:12-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wafalme wa dunia hawakusadiki, Wala wote wakaao duniani, Ya kwamba mtesi na adui wangeingia Katika malango ya Yerusalemu. Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake Na maovu ya makuhani wake, Walioimwaga damu ya wenye haki Katikati yake. Hutanga-tanga njiani kama vipofu, Wametiwa unajisi kwa damu; Hata ikawa watu wasiweze Kuyagusa mavazi yao. Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu, Ondokeni, ondokeni, msiguse; Walipokimbia na kutanga-tanga, watu walisema kati ya mataifa, Hawatakaa hapa tena. Hasira ya BWANA imewatenga, Yeye hatawaangalia tena; Hawakujali nafsi za wale makuhani, Hawakuwaheshimu wazee wao. Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa. Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika. Waliotufuatia ni wepesi Kuliko tai za mbinguni; Hao walitufuatia milimani, Nao walituotea jangwani. Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA, Alikamatwa katika marima yao; Ambaye kwa habari zake tulisema, Chini ya kivuli chake tutakaa kati ya mataifa. Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu, Ukaaye katika nchi ya Usi; Hata kwako kikombe kitapita, Utalewa, na kujifanya uchi. Uovu wako umetimia, Ee binti Sayuni; Hatakuhamisha tena; Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu; Atazivumbua dhambi zako.
Maombolezo 4:12-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wafalme wa dunia hawakuamini, wala mtu yeyote wa duniani, kwamba adui na watesi wangeweza kuingia kwenye malango ya Yerusalemu. Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake, na maovu ya makuhani wake, waliomwaga ndani yake damu ya wenye haki. Sasa wanapapasa papasa barabarani kama watu ambao ni vipofu. Wamenajisiwa kabisa kwa damu, hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao. Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi! Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!” Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko, watu miongoni mwa mataifa wanasema, “Hawawezi kukaa hapa zaidi.” BWANA mwenyewe amewatawanya; hawaangalii tena. Makuhani hawaonyeshwi heshima, wazee hawakubaliki. Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka, kwa kutazamia bure msaada; tuliangalia kutoka minara yetu kwa taifa lisiloweza kutuokoa. Watu walituvizia katika kila hatua hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu. Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia, kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika. Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai angani; walitusaka juu milimani na kutuvizia jangwani. Mpakwa mafuta wa BWANA, pumzi ya uhai wetu hasa, alinaswa katika mitego yao. Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa. Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu, wewe unayeishi nchi ya Usi. Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa, Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi. Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha, hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni. Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako, na atafunua uovu wako.
Maombolezo 4:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Wafalme duniani hawakuamini wala wakazi wowote wa ulimwenguni, kwamba mvamizi au adui angeweza kuingia malango ya Yerusalemu. Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake, yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake. Walitangatanga barabarani kama vipofu, walikuwa wamekuwa najisi kwa damu, hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa. Watu waliwapigia kelele wakisema: “Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi! Tokeni, tokeni, msiguse chochote.” Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga; watu wa mataifa walitamka: “Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!” Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya, wala hatawajali tena. Makuhani hawatapata tena heshima, wazee hawatapendelewa tena. Tulichoka kukaa macho kungojea msaada; tulikesha na kungojea kwa hamu taifa ambalo halikuweza kutuokoa. Watu walifuatilia hatua zetu, tukashindwa kupita katika barabara zetu. Siku zetu zikawa zimetimia; mwisho wetu ukawa umefika. Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai, walitukimbiza milimani, walituvizia huko nyikani. Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea, yule mfalme aliyewekwa wakfu wa Mwenyezi-Mungu, yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake tutaishi miongoni mwa mataifa.” Wakazi wa Edomu, mwaweza kushangilia kwa sasa, mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi; lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia, nanyi pia mtakinywa na kulewa, hata mtayavua mavazi yenu! Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika; Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni. Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu, atazifichua dhambi zenu.
Maombolezo 4:12-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wafalme wa dunia hawakusadiki, Wala wote wakaao duniani, Ya kwamba mtesi na adui wangeingia Katika malango ya Yerusalemu. Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake Na maovu ya makuhani wake, Walioimwaga damu ya wenye haki Katikati yake. Hutangatanga njiani kama vipofu, Wametiwa unajisi kwa damu; Hata ikawa hakuna aliyeweza Kuyagusa mavazi yao. Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu, Ondokeni, ondokeni, msiguse; Walipokimbia na kutangatanga, watu walisema kati ya mataifa, Hawatakaa hapa tena. Hasira ya BWANA imewatenga, Yeye hatawaangalia tena; Hawakujali nafsi za wale makuhani, Hawakuwaheshimu wazee wao. Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa. Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika. Waliotufuatia ni wepesi Kuliko tai za mbinguni; Hao walitufuatia milimani, Nao walituotea jangwani. Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA, Alikamatwa katika marima yao; Ambaye kwa habari zake tulisema, Chini ya kivuli chake tutakaa kati ya mataifa. Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu, Ukaaye katika nchi ya Usi; Hata kwako kikombe kitapita, Utalewa, na kujifanya uchi. Adhabu ya uovu wako imetimia, Ee binti Sayuni; Hatakuhamisha tena; Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu; Atazivumbua dhambi zako.