Maombolezo 4
4
# 4 Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. 1 Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake,
dhahabu iliyo safi haingʼai!
Vito vya thamani vimetawanywa
kwenye mwanzo wa kila barabara.
2 Wana wa Sayuni wenye thamani,
ambao mwanzo uzito wa thamani yao
ulikuwa wa dhahabu,
sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3 Hata mbweha hutoa matiti yao
kunyonyesha watoto wao,
lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma
kama mbuni jangwani.
4 Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,
watoto huomba mkate,
lakini hakuna yeyote awapaye.
5 Wale waliokula vyakula vya kifahari
ni maskini barabarani.
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau
sasa wanalalia majivu.
6 Adhabu ya watu wangu
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,
ambayo ilipinduliwa ghafula
bila kuwepo mkono wa msaada.
7Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji
na weupe kuliko maziwa,
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,
kuonekana kwao kama yakuti samawi.
8 Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;
hawatambulikani barabarani.
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,
imekuwa mikavu kama fimbo.
9 Wale waliouawa kwa upanga ni bora
kuliko wale wanaokufa njaa;
wanateseka kwa njaa, wanatokomea
kwa kukosa chakula kutoka shambani.
10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma
wanapika watoto wao wenyewe,
waliokuwa chakula chao
watu wangu walipoangamizwa.
11 Bwana ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;
ameimwaga hasira yake kali.
Amewasha moto katika Sayuni
ambao umeteketeza misingi yake.
12 Wafalme wa dunia hawakuamini,
wala mtu yeyote wa duniani,
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia
kwenye malango ya Yerusalemu.
13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,
na maovu ya makuhani wake,
waliomwaga ndani yake
damu ya wenye haki.
14 Sasa wanapapasa papasa barabarani
kama watu ambao ni vipofu.
Wamenajisiwa kabisa kwa damu,
hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.
15 Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”
Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko,
watu miongoni mwa mataifa wanasema,
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”
16 Bwana mwenyewe amewatawanya;
hawaangalii tena.
Makuhani hawaonyeshwi heshima,
wazee hawakubaliki.
17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,
kwa kutazamia bure msaada;
tuliangalia kutoka minara yetu
kwa taifa lisiloweza kutuokoa.
18 Watu walituvizia katika kila hatua
hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.
19 Waliotufuatia walikuwa wepesi
kuliko tai angani;
walitusaka juu milimani
na kutuvizia jangwani.
20 Mpakwa mafuta wa Bwana, pumzi ya uhai wetu hasa,
alinaswa katika mitego yao.
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake
tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.
21 Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,
wewe unayeishi nchi ya Usi.
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,
hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.
Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako,
na atafunua uovu wako.
Iliyochaguliwa sasa
Maombolezo 4: NEN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.