Yoshua 17:3-6
Yoshua 17:3-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “BWANA alimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la BWANA. Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.
Yoshua 17:3-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na watoto wa kiume, bali alikuwa na watoto wa kike tu, nao walikuwa: Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirza. Mabinti hao wakamjia kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, na viongozi wengine wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwamuru Mose atugawie na sisi sote nchi kama wagawiwavyo wanaume wa kabila letu.” Basi kufuatana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Yoshua akawapatia sehemu yao kama alivyowapa wanaume wa kabila lao. Kwa hiyo kabila la Manase liliongezewa sehemu mbili zaidi yaani nchi ya Gileadi na Bashani iliyoko upande mwingine wa mto Yordani, kwa sababu binti za Manase waligawiwa sehemu zao kama walivyogawiwa wanaume wa kabila lao. (Nchi ya Gileadi walipewa wazawa wengine wa Manase).
Yoshua 17:3-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana wa kiume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, Nuhu, Hogla, Milka na Tirza. Nao wakaja mbele ya kuhani Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya viongozi, wakasema, BWANA alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuifuata hiyo amri ya BWANA akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao. Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng'ambo ya Yordani; kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe wa kiume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana wa kiume wa Manase waliosalia.
Yoshua 17:3-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, BWANA alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya BWANA akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao. Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng’ambo ya Yordani; kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia.