Yobu 40:15-24
Yobu 40:15-24 Biblia Habari Njema (BHN)
“Liangalie lile dude Behemothi, nililoliumba kama nilivyokuumba wewe. Hilo hula nyasi kama ng'ombe, lakini mwilini lina nguvu ajabu, na misuli ya tumbo lake ni imara. Huufanya mkia wake mgumu kama mwerezi, mishipa ya mapaja yake imeshonwa pamoja. Mifupa yake ni mabomba ya shaba, viungo vyake ni kama pao za chuma. “Hilo ni la kwanza la ajabu kati ya viumbe vyangu! Ni mimi Muumba wake niwezaye kulishinda. Milima wanamocheza wanyama wote wa porini hutoa chakula chake. Hujilaza chini ya vichaka vya miiba, na kujificha kati ya matete mabwawani. Hujisitiri katika vivuli vya vichaka vya miiba na vya miti iotayo kando ya vijito. Mto ukifurika haliogopi, halitishiki hata mto Yordani ukilifurikia kinywani. Nani awezaye kuliziba macho na kuliteka? Nani awezaye kulitoboa pua kwa mtego?
Yobu 40:15-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe; Yeye hula nyasi kama ng'ombe, Tazama basi, nguvu zake zimo katika viuno vyake, Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake. Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi; Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja. Mifupa yake ni kama mirija ya shaba; Mbavu zake ni kama vipande vya chuma. Yeye ni wa kwanza kwa hayo matendo makuu ya Mungu; Ni Muumba wake tu awezaye kumkabili kwa upanga wake. Hakika milima humtolea chakula; Hapo wachezapo wanyama pori wote. Hulala chini ya miti yenye vivuli, Mafichoni penye mianzi, na matopeni. Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao; Mierebi ya vijito humzunguka. Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki; Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake. Je! Mtu yeyote atamnasa akiwa yu macho, Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?
Yobu 40:15-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe; Yeye hula nyasi kama vile ng’ombe, Tazama basi, nguvu zake ni katika viuno vyake, Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake. Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi; Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja. Mifupa yake ni kama mirija ya shaba; Mbavu zake ni kama vipande vya chuma. Yeye ni mkuu wa njia za Mungu; Yeye aliyemfanya alimpa upanga wake. Hakika milima humtolea chakula; Hapo wachezapo wanyama wote wa barani. Hulala chini ya miti yenye vivuli, Mafichoni penye mianzi, na matopeni. Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao; Mierebi ya vijito humzunguka. Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki; Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake. Je! Mtu ye yote atamnasa akiwa yu macho, Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?
Yobu 40:15-24 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Mwangalie mnyama aitwaye Behemothi, niliyemuumba kama nilivyokuumba wewe, anayekula majani kama ng’ombe. Tazama basi nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake, uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake! Mkia wake hutikisika kama mwerezi; mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja. Mifupa yake ni bomba za shaba, maungo yake ni kama fito za chuma. Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu, lakini Muumba wake anaweza kumsogelea kwa upanga wake. Vilima humletea yeye mazao yake, nao wanyama pori wote hucheza karibu naye. Hulala chini ya mimea ya yungiyungi, katika maficho ya matete kwenye matope. Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake; miti mirefu karibu na kijito humzunguka. Mto unapofurika, yeye hapati mshtuko wa hofu; yeye yu salama, hata kama Yordani ingefurika hadi kwenye kinywa chake. Je, mtu yeyote anaweza kumkamata yeye akiwa macho, au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?