Yobu 38:1-18
Yobu 38:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Mwenyezi-Mungu alimjibu Yobu kutoka dhoruba: “Nani wewe unayevuruga mashauri yangu kwa maneno yasiyo na akili? Jikaze kama mwanamume, nami nitakuuliza nawe utanijibu. “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya dunia? Niambie, kama una maarifa. Ni nani aliyeweka vipimo vyake, wajua bila shaka! Au nani aliyelaza kamba juu yake kuipima? Je, nguzo za dunia zimesimikwa juu ya nini, au nani aliyeliweka jiwe lake la msingi, nyota za asubuhi zilipokuwa zikiimba pamoja, na wana wa Mungu wakapaza sauti za shangwe? Ni nani aliyeyafunga mafuriko ya bahari wakati yalipozuka na kuvuma kutoka vilindini? Mimi ndiye niliyeifunika bahari kwa mawingu na kuiviringishia giza nene. Niliiwekea bahari mipaka, nikaizuia kwa makomeo na milango, nikaiambia: ‘Mwisho wako ni hapa, si zaidi! Mawimbi yako ya nguvu yatakomea hapa!’ “Yobu, tangu uzaliwe umewahi kuamuru kupambazuke? na kulifanya pambazuko lijue mahali pake, ili lipate kuikamata dunia kwa pembe zake na kuwatimulia mbali waovu waliomo? Dunia hugeuka na kupata rangi kama vazi; kama udongo wa mfinyanzi unavyogeuzwa na mhuri. Lakini waovu watanyimwa mwanga wao, mkono wanaonyosha kupiga watu utavunjwa. “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? au kutembea juu ya sakafu ya kilindi cha bahari? Je, umewahi kuoneshwa malango ya kifo, au kuyaona malango ya makazi ya giza nene? Je, wajua ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote.
Yobu 38:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye ushauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno kama mwanamume, Maana nitakuuliza neno, nawe niambie. Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama una ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake – hakika unajua! Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha? Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipotoka kwa nguvu kama kwamba imetoka tumboni mwa nchi. Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango, Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yenye nguvu yatazuiliwa? Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung'utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya mhuri, Vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, Na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote.
Yobu 38:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo BWANA akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno kama mwanamume, Maana nitakuuliza neno, nawe niambie. Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha? Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango, Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa? Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, Vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, Na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote.
Yobu 38:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha BWANA akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema: “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza swali, nawe unijibu. “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia? Niambie, kama unafahamu. Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake? Hakika wewe unajua! Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake? Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini, au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni, wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha? “Ni nani aliyeifungia bahari milango ilipopasuka kutoka tumbo, nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake, na kuyafungia katika giza nene, nilipoamuru mipaka yake, na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake, niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi; hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’? “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke, au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake, yapate kushika miisho ya dunia, na kuwakungʼuta waovu waliomo? Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri; sura yake hukaa kama ile ya vazi. Waovu huzuiliwa nuru yao, nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa. “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi? Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti? Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti? Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote.