Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 32:1-14

Yobu 32:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe. Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu. Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu. Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kumliko yeye. Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka. Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri, nanyi ni wazee; ndiyo sababu niliogopa, sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua. Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme, nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’ Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu. Sio wazee peke yao walio na hekima, sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa. “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi; mimi nami nitawaambia lile ninalojua. Nilingojea mlipokuwa mnaongea, nilizisikiliza hoja zenu; mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema, niliwasikiliza kwa makini. Lakini hakuna hata mmoja wenu aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa; hakuna hata mmoja wenu aliyeweza kujibu hoja zake. Msiseme, ‘Tumepata hekima; Mungu na amthibitishe kuwa mwongo, wala si mwanadamu.’ Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu, nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.

Shirikisha
Soma Yobu 32

Yobu 32:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema. Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama, akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu. Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa. Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao. Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira. Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema: “Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi; kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu. Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme, wenye miaka mingi wafundishe hekima.’ Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu, hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu, ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu. Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekima wala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa. Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni, acheni nami nitoe maoni yangu.’ “Basi, mimi nilingojea mlichotaka kusema, nilisikiliza misemo yenu ya hekima, mlipokuwa mnajaribu kutafuta la kusema. Niliwasikiliza kwa makini sana, lakini hakuna mmoja wenu aliyemshinda Yobu; nyote mlishindwa kuyajibu maneno yake. Jihadharini msije mkasema, ‘Sasa tumepata hekima. Atakayemshinda ni Mungu, sio binadamu.’ Maneno ya Yobu hayakuwa kwa ajili yangu, kwa hiyo sitamjibu kama mlivyomjibu nyinyi.

Shirikisha
Soma Yobu 32