Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 32:1-14

Ayubu 32:1-14 NEN

Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe. Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu. Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu. Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kumliko yeye. Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka. Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri, nanyi ni wazee; ndiyo sababu niliogopa, sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua. Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme, nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’ Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu. Sio wazee peke yao walio na hekima, sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa. “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi; mimi nami nitawaambia lile ninalojua. Nilingojea mlipokuwa mnaongea, nilizisikiliza hoja zenu; mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema, niliwasikiliza kwa makini. Lakini hakuna hata mmoja wenu aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa; hakuna hata mmoja wenu aliyeweza kujibu hoja zake. Msiseme, ‘Tumepata hekima; Mungu na amthibitishe kuwa mwongo, wala si mwanadamu.’ Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu, nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.