Yobu 16:1-22
Yobu 16:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Yobu akajibu: “Mambo kama hayo nimeyasikia mengi; nyinyi ni wafariji duni kabisa! Mwisho wa maneno haya matupu ni lini? Au ni kitu gani kinachowachochea kujibu? Kama nyinyi mngekuwa mimi, na mimi nyinyi, ningeweza kusema kama nyinyi ningeweza kubuni maneno dhidi yenu, na kutikisa kichwa changu. Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu, na maneno yangu ya faraja yangewatuliza. “Lakini nikisema maumivu yangu hayatulii, na nikikaa kimya hayaondoki. Kweli Mungu amenichakaza ameharibu kila kitu karibu nami. Amenifanya ninyauke, na huo ni ushindi dhidi yangu. Kukonda kwangu kumenikabili na kushuhudia dhidi yangu. Amenirarua kwa hasira na kunichukia; amenisagia meno; na adui yangu ananikodolea macho. Watu wananidhihaki na kunicheka; makundi kwa makundi hunizunguka, na kunipiga makofi mashavuni. Mungu amenitia mikononi mwa wajeuri, na kunitupa mikononi mwa waovu. Nilikuwa nimestarehe, lakini akanivunjavunja, alinikaba shingo na kunipasua vipandevipande; alinifanya shabaha ya mishale yake, akanipiga mishale kutoka kila upande. Amenipasua figo bila huruma, na nyongo yangu akaimwaga chini. Hunivunja na kunipiga tena na tena; hunishambulia kama askari. “Nimejishonea mavazi ya gunia, fahari yangu nimeibwaga mavumbini. Uso wangu ni mwekundu kwa kulia, kope zangu zimekuwa nyeusi ti; ingawa sijafanya dhuluma kwa mkono wangu, na sala zangu kwa Mungu ni safi. “Ewe dunia, usiifunike damu yangu iliyomwagika; kilio changu kienee kila mahali. Nina hakika ninaye shahidi wangu mbinguni, mwenye kunitetea yuko huko juu. Rafiki zangu wanidharau; nabubujika machozi kumwomba Mungu. Laiti mtu angenitetea mbele ya Mungu, kama ifanyikavyo duniani kati za watu wawili. Naam, miaka yangu ni michache, nami nitakwenda huko ambako sitarudi.
Yobu 16:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na maliwazo ya midomo yangu yangewatuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa. Umenishika sana, na kuwa ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu. Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesagasaga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali. Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hukutana pamoja juu yangu. Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu. Nilikuwa katika raha, naye akanivunjavunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake. Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua figo zangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi. Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa. Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na nguvu zangu nimezibwaga mavumbini. Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu liko katika kope zangu; Ijapokuwa hakuna udhalimu mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi. Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika. Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu. Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi; Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake. Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena.
Yobu 16:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa. Umenishika sana, ni ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu. Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesaga-saga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali. Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hujikutanisha pamoja juu yangu. Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu. Nilikuwa katika raha, naye akanivunja-vunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake. Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua viuno vyangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi. Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa. Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na pembe yangu nimeidhili uvumbini. Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu li katika kope zangu; Ijapokuwa hapana jeuri mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi. Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika. Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu. Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi; Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake. Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena.
Yobu 16:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Ayubu akajibu: “Nimepata kusikia mambo mengi kama haya, nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha! Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho? Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno? Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi, kama mngekuwa katika hali yangu; ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu, na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini kinywa changu kingewatia moyo; faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu. “Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi; nami kama nikijizuia, wala hayaondoki. Ee Mungu, hakika umenichakaza; umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote. Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi; nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu. Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake, na kunisagia meno yake; adui yangu hunikazia macho yake makali. Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki; hunipiga shavuni mwangu kwa dharau, na kuungana pamoja dhidi yangu. Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya, na kunitupa katika makucha ya waovu. Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja; amenikamata shingo na kuniponda. Amenifanya mimi kuwa shabaha yake; wapiga upinde wake wananizunguka. Bila huruma, huchoma figo zangu, na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi. Huniponda tena na tena; hunishambulia kama shujaa wa vita. “Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi. Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia, macho yangu yamepigwa na giza kuu. Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri, na maombi yangu ni safi. “Ee nchi, usiifunike damu yangu, nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe. Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni; wakili wangu yuko juu. Mwombezi wangu ni rafiki yangu macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu; kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake. “Ni miaka michache tu itapita kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.