Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 16:1-22

Ayubu 16:1-22 SRUV

Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha. Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu? Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu. Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na maliwazo ya midomo yangu yangewatuliza. Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani? Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa. Umenishika sana, na kuwa ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu. Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesagasaga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali. Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hukutana pamoja juu yangu. Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu. Nilikuwa katika raha, naye akanivunjavunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake. Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua figo zangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi. Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa. Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na nguvu zangu nimezibwaga mavumbini. Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu liko katika kope zangu; Ijapokuwa hakuna udhalimu mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi. Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika. Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu. Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi; Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake. Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena.

Soma Ayubu 16