Yohane 7:1-9
Yohane 7:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea huko Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumuua. Sikukuu ya Wayahudi ya vibanda ilikuwa imekaribia. Basi, ndugu zake wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya. Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadamu unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu.” (Hata ndugu zake hawakumwamini). Basi, Yesu akawaambia, “Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu nyinyi kila wakati unafaa. Ulimwengu hauwezi kuwachukia nyinyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nashuhudia juu yake kwamba matendo yake ni maovu. Nyinyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika.” Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
Yohane 7:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Yudea, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitaka kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, sikukuu ya vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Yudea, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye mambo kwa siri, naye yeye mwenyewe anataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Wakati wangu haujafika bado; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. Pandeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sipandi bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa wakati wangu haujatimia. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alibaki huko Galilaya.
Yohane 7:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini. Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu. Kweeni ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa haujatimia wakati wangu. Naye alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya.
Yohane 7:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya mambo haya, Yesu alikwenda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Uyahudi kwa sababu Wayahudi huko walitaka kumuua. Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya. Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jionyeshe kwa ulimwengu.” Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini. Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu. Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.” Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.