Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 4:31-54

Yohane 4:31-54 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.” Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?” Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake. Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa. Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uhai wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna.’ Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho; wengine walifanya kazi, lakini nyinyi mnafaidika kutokana na jasho lao.” Wasamaria wengi wa kijiji kile walimwamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.” Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. Watu wengi zaidi waliamini kwa sababu ya ujumbe wake. Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.” Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.” Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!” Huyo ofisa akamwambia, “Bwana, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao ataishi.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake. Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.” Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao ataishi.” Hapo yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.

Shirikisha
Soma Yohane 4

Yohane 4:31-54 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenituma, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yanakuja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi niliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena tunajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na ofisa mmoja ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Yudea mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa karibu kufa. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule ofisa akamwambia, Bwana, ushuke mtoto wangu asije akafa. Yesu akamwambia, Nenda; mwanao yu hai. Mtu yule akaliamini lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Na alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa na nafuu; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake. Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Yudea kwenda Galilaya.

Shirikisha
Soma Yohane 4

Yohane 4:31-54 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao. Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa? Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu. Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha. Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake. Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

Shirikisha
Soma Yohane 4

Yohane 4:31-54 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Mwalimu, kula.” Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.” Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune’? Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. Hivyo ule msemo, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda. Wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.” Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini. Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.” Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu. Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa. Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.” Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.” Isa akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake. Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.” Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa. Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.

Shirikisha
Soma Yohane 4