Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 4:31-54

Yohana 4:31-54 NENO

Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Mwalimu, kula.” Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.” Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune’? Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. Hivyo ule msemo, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda. Wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.” Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini. Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.” Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu. Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa. Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.” Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.” Isa akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake. Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.” Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa. Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.