Waamuzi 5:1-31
Waamuzi 5:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyo, Debora na Baraki, mwana wa Abinoamu, wakaimba wimbo huu: “Viongozi walijitokeza kuongoza Israeli, watu walijitolea kwa hiari yao. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu! “Sikilizeni, enyi wafalme! Tegeni sikio, enyi wakuu! Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. “Ee Mwenyezi-Mungu, ulipotoka huko Seiri, ulipoteremka mlimani Edomu, nchi ilitetemeka, mbingu zilidondosha maji, naam, mawingu yakaiangusha mvua. Milima ilitikisika mbele yako Mwenyezi-Mungu, naam, mlima Sinai mbele yako Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. “Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, katika wakati wa Yaeli, misafara ilikoma kupita nchini, wasafiri walipitia vichochoroni. Wakulima walikoma kuwako, walikoma kuwako katika Israeli, mpaka nilipotokea mimi Debora, mimi niliye kama mama wa Israeli. Walijichagulia miungu mipya, kukawa na vita katika nchi. Lakini hakukupatikana mwenye upanga au ngao kati ya watu 40,000 wa Israeli. Nawapa heshima makamanda wa Israeli waliojitoa kwa hiari yao kati ya watu. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu! “Tangazeni, enyi wapandapunda weupe, enyi mnaokalia mazulia ya fahari, nyinyi mnaotembea njiani, tangazeni jambo hilo. Imbeni kupita wanamuziki kwenye visima vya maji, tangazeni ushindi wa Mwenyezi-Mungu, ushindi kwa wakulima wake katika Israeli. Ndipo watu wa Mwenyezi-Mungu waliposhuka malangoni. “Amka, amka, Debora! Amka! Amka uimbe wimbo! Amka, Baraki mwana wa Abinoamu, uwachukue mateka wako. Mashujaa waliobaki waliteremka, watu wa Mwenyezi-Mungu walikwenda kumpigania dhidi ya wenye nguvu. Kutoka Efraimu waliteremka bondeni, wakafuata ndugu zao watu wa Benyamini; kutoka Makiri walishuka makamanda, kutoka Zebuluni maofisa wakuu. Wakuu wa Isakari wakafuatana na Debora, watu wa Isakari waaminifu kwa Baraki; wakamfuata mbio mpaka bondeni. Lakini miongoni mwa koo za Reubeni kulikuwamo kusitasita kwingi. Kwa nini walibaki mazizini? Ili kusikiliza milio ya kondoo? Miongoni mwa koo za Reubeni kulikuwamo kusitasita kwingi. Kabila la Gileadi lilibaki ngambo ya Yordani. Kabila la Dani, kwa nini mlibaki merikebuni? Kabila la Asheri lilitulia huko pwani ya bahari, lilikaa bandarini mwake. Watu wa Zebuluni ni watu waliohatarisha maisha yao katika kifo. Hata wa Naftali walikikabili kifo kwenye miinuko ya mashamba. “Huko Taanaki, kando ya chemchemi za Megido, wafalme walikuja, wakapigana; wafalme wa Kanaani walipigana, lakini hawakupata nyara za fedha. Nyota kutoka mbinguni zilishiriki vita, zilifuata njia zao, zilipigana na Sisera. Mafuriko ya mto Kishoni yaliwachukua mbali, naam, mafuriko makali ya mto Kishoni. Songa mbele kwa nguvu, ee nafsi yangu! “Farasi walipita wakipiga shoti;, walikwenda shoti na kishindo cha kwato zao. Malaika wa Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Uapizeni mji wa Merosi, waapizeni vikali wakazi wake; maana hawakuja kumsaidia Mwenyezi-Mungu hawakumsaidia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wenye nguvu’. “Abarikiwe kuliko wanawake wote Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Naam, amebarikiwa kuliko wanawake wote wanaokaa mahemani. Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa; alimletea siagi katika bakuli ya heshima. Kwa mkono mmoja alishika kigingi cha hema, na kwa mkono wake wa kulia nyundo ya fundi; alimponda Sisera kichwa, alivunja na kupasuapasua paji lake. Sisera aliinama, akaanguka; alilala kimya miguuni pake. Hapo alipoinama ndipo alipoanguka, amekufa! “Mama yake Sisera alitazama dirishani alichungulia katika viunzi vyake, akalalamika: ‘Kwa nini gari lake limechelewa? Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa kusikika?’ Jibu akalipata kwa wanawake wenye hekima: Akajituliza tena na tena kwa jibu hilo: ‘Bila shaka wanatafuta na kugawana nyara; msichana mmoja au wawili kwa kila askari, vazi la sufu ya rangi kwa ajili ya Sisera. Vazi la sufu iliyotariziwa, na mikufu miwili ya nakshi kwa ajili ya shingo yangu!’ “Ee Mwenyezi-Mungu, waangamie adui zako wote! Lakini rafiki zako na wawe kama jua, wakati linapochomoza kwa mwanga mkubwa!” Nayo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.
Waamuzi 5:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema; Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini BWANA. Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia BWANA; Nitamhimidi BWANA, Mungu wa Israeli. BWANA, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondosha maji, Naam, mawingu yakadondosha maji. Milima ikayeyuka mbele za uso wa BWANA, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa BWANA, Mungu wa Israeli. Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nayo misafara ilipita kwa njia za kando. Watawala walikoma katika Israeli, walikoma, Hadi mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli. Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arubaini wa Israeli? Moyo wangu unawaelekea makamanda wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini BWANA. Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu. Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya BWANA; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa BWANA waliposhuka malangoni. Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu. Ndipo waliteremka mabaki ya waungwana na ya watu; BWANA alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa. Kutoka Efraimu waliteremka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka makamanda, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi. Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake. Zabuloni ndio watu waliohatarisha roho zao hadi kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni. Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yoyote ya fedha. Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera. Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu. Kisha, kwa kishindo kwato za farasi zilipigapiga, Kwa maana walivyoenda shoti, Walipowakimbiza farasi wenye nguvu. Ulaanini Merozi, alisema malaika wa BWANA, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia BWANA, Kumsaidia BWANA juu ya hao wenye nguvu. Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani. Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima. Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kulia ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake. Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa. Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia? Mabibi wake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa jawabu. Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbalimbali, Nyara za mavazi ya rangi mbalimbali ya darizi; Ya rangi mbalimbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka. Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA. Bali wao wampendao na wawe kama jua hapo litokapo kwa nguvu zake. Nayo nchi ikastarehe miaka arubaini.
Waamuzi 5:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema; Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini BWANA. Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia BWANA; Nitamhimidi BWANA, Mungu wa Israeli. BWANA, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji. Milima ikayeyuka mbele za uso wa BWANA, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa BWANA, Mungu wa Israeli. Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando. Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli. Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli? Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini BWANA. Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu. Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya BWANA; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa BWANA waliposhuka malangoni. Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu. Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; BWANA alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa. Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi. Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. Gileadi alikaa ng’ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake. Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni. Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha. Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera. Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu. Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu. Ulaanini Merozi, alisema malaika wa BWANA, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia BWANA, Kumsaidia BWANA juu ya hao wenye nguvu. Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani. Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima. Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake. Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa. Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia? Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu. Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka. Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA. Bali wao wampendao na wawe kama jua hapo litokapo kwa nguvu zake. Nayo nchi ikastarehe miaka arobaini.
Waamuzi 5:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Debora na Baraka mwana wa Abinoamu wakaimba wimbo huu: “Wakuu katika Israeli wanapoongoza, wakati watu wanapojitoa kwa hiari yao wenyewe: mhimidini BWANA! “Sikieni hili, enyi wafalme! Sikilizeni, enyi watawala! Nitamwimbia BWANA, nitaimba; kwa wimbo nitamhimidi BWANA, Mungu wa Israeli. “Ee BWANA, ulipotoka katika Seiri, ulipopita katika mashamba ya Edomu, nchi ilitetemeka, mbingu nazo zikamwaga, naam, mawingu yakamwaga maji. Milima ilitetemeka mbele za BWANA, hata ule wa Sinai, mbele za BWANA, Mungu wa Israeli. “Katika siku za Shamgari mwana wa Anathi, katika siku za Yaeli, barabara kuu hazikuwa na watu; wasafiri walipita njia za kando. Mashujaa walikoma katika Israeli, walikoma mpaka mimi, Debora, nilipoinuka, nilipoinuka kama mama katika Israeli. Walipochagua miungu migeni, vita vilikuja katika malango ya mji, hapakuonekana ngao wala mkuki miongoni mwa mashujaa 40,000 katika Israeli. Moyo wangu u pamoja na wakuu wa Israeli, pamoja na wale wanaojitoa wenyewe kwa hiari yao miongoni mwa watu. Mhimidini BWANA! “Nanyi mpandao punda weupe, mkiketi juu ya matandiko ya thamani, nanyi mtembeao barabarani, fikirini juu ya sauti za waimbaji mahali pa kunyweshea maji. Wanasimulia matendo ya haki ya BWANA, matendo ya haki ya mashujaa wake katika Israeli. “Ndipo watu wa BWANA walipoteremka malangoni pa mji. ‘Amka, amka! Debora! Amka, amka, uimbe! Ee Baraka! Inuka, chukua mateka wako uliowateka, ee mwana wa Abinoamu.’ “Ndipo mabaki ya watu wakashuka dhidi ya wenye nguvu, watu wa BWANA, wakashuka dhidi ya mashujaa wenye nguvu. Kutoka Efraimu wakaja watu, ambao chimbuko lao ni Amaleki; Benyamini akiwa miongoni mwa watu waliokufuata. Kutoka Makiri wakashuka viongozi, na kutoka Zabuloni wale washikao fimbo ya jemadari. Wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora; naam, Isakari alikuwa pamoja na Baraka, wakija nyuma yake kwa mbio wakielekea bondeni. Katika jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni. Kwa nini ulikaa katikati ya mazizi ya kondoo kusikiliza sauti ya filimbi zinazoita makundi? Kwa jamaa za Reubeni, palikuwa na kujihoji kukubwa moyoni. Gileadi alikaa ngʼambo ya Yordani. Naye Dani, kwa nini alikaa kwenye merikebu siku nyingi? Asheri alikaa kwa utulivu ufuoni mwa bahari, akikaa kwenye ghuba zake ndogo. Watu wa Zabuloni walihatarisha maisha yao, vilevile nao watu wa Naftali. “Wafalme walikuja na kufanya vita; wafalme wa Kanaani walipigana huko Taanaki karibu na maji ya Megido, lakini hawakuchukua fedha wala nyara. Kutoka mbinguni nyota zilipigana, nyota kutoka njia zake zilipigana na Sisera. Mto wa Kishoni uliwasomba, ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Songa mbele, ee nafsi yangu, kwa ujasiri! Ndipo kwato za farasi zikafanya mshindo: farasi wake wenye nguvu huenda mbio kwa kurukaruka. Malaika wa BWANA akasema, ‘Merozi alaaniwe. Walaaniwe watu wake kwa uchungu, kwa kuwa hawakuja kumsaidia BWANA, kumsaidia BWANA dhidi ya hao wenye nguvu.’ “Yaeli abarikiwe kuliko wanawake wote, mkewe Heberi, Mkeni, abarikiwe kuliko wanawake wote waishio kwenye mahema. Aliomba maji, naye akampa maziwa; kwenye bakuli la heshima akamletea maziwa mgando. Akanyoosha mkono wake akashika kigingi cha hema, mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi. Akampiga Sisera kwa nyundo, akamponda kichwa chake, akamvunjavunja na kumtoboa paji lake la uso. Aliinama miguuni pa Yaeli, akaanguka; akalala hapo. Pale alipoinama miguuni pake, alianguka; pale alipoinamia, ndipo alipoanguka, akiwa amekufa. “Kupitia dirishani mamaye Sisera alichungulia; nyuma ya dirisha alilia, akasema, ‘Mbona gari lake linachelewa kufika? Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa?’ Wanawake wenye busara kuliko wengine wote wakamjibu; naam, husema moyoni mwake, ‘Je, hawapati na kugawanya nyara: msichana mmoja au wawili kwa kila mtu, mavazi ya rangi mbalimbali kwa Sisera kuwa nyara, mavazi ya rangi mbalimbali yaliyotariziwa, mavazi yaliyotariziwa vizuri kwa ajili ya shingo yangu: yote haya yakiwa nyara?’ “Adui zako wote na waangamie, Ee BWANA! Bali wote wakupendao na wawe kama jua lichomozavyo kwa nguvu zake.” Hivyo nchi ikawa na amani kwa miaka arobaini.