Isaya 51:1-16
Isaya 51:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa, nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu. Utazameni mwamba mlimochongwa, chimbo la mawe mlimochimbuliwa. Mkumbukeni Abrahamu babu yenu, na Sara aliyewazaa nyinyi. Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita, lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi. “Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni, nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika. Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni, majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu. Kwake kutapatikana furaha na shangwe, na nyimbo za shukrani zitasikika humo. “Nisikilizeni enyi watu wangu, nitegeeni sikio enyi taifa langu. Sheria na haki zitatoka kwangu mimi; nazo zitakuwa mwanga wa mataifa. Nitaleta ukombozi hima; wokovu nitakaoleta waanza kutokea. Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa. Wakazi wa nchi za mbali wananingojea, wanaitegemea nguvu yangu. Inueni macho mzitazame mbingu, kisha tazameni dunia huko chini. Mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake watakufa kama wadudu. Lakini wokovu niuletao wadumu milele; ukombozi wangu kamwe hautakoma. “Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki, ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu. Msiogope dharau za watu, wala kufadhaishwa na masimango yao. Maana wataliwa na nondo kama vile vazi; viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu. Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele; wokovu wangu hautakuwa na mwisho.” Amka! Amka ee Mwenyezi-Mungu! Jivike nguvu zako utuokoe. Amka kama ulivyofanya hapo zamani, nyakati za vizazi vya hapo kale. Je, si wewe uliyemkatakata Rahabu, ukalitumbua dude hilo la kutisha? Wewe ndiwe uliyeikausha bahari, ndiwe uliyevikausha vilindi vya maji, ukafanya njia katika vilindi vya bahari, ili wale uliowakomboa wavuke humo. Watu wako uliowakomboa, ee Mwenyezi-Mungu, watarudi, watakuja Siyoni wakiimba; watajaa furaha ya milele, watapata furaha na shangwe. Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji. Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa, binadamu ambaye hutoweka kama nyasi? Wewe umenisahau mimi Mwenyezi-Mungu Muumba wako, niliyezitandaza mbingu, na kuiweka misingi ya dunia! Wewe waendelea kuogopa siku zote, kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu wako, kwamba yuko tayari kukuangamiza! Lakini hasira yake itafika wapi? Wanaodhulumiwa watafunguliwa hima, hawatakufa na kushuka shimoni, wala hawatatindikiwa chakula. Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; nivurugaye bahari, mawimbi yake yakanguruma; Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina langu! Nimeyaweka maneno yangu mdomoni mwako; nimekuficha katika kivuli cha mkono wangu. Mimi nilizitandaza mbingu, nikaiweka misingi ya dunia. Mimi nawaambieni enyi watu wa Siyoni: ‘Nyinyi ni watu wangu.’”
Isaya 51:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta BWANA; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa. Mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nilimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi. Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya nyika yake kuwa kama bustani ya Edeni, na jangwa lake kama bustani ya BWANA; shangwe na furaha zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba. Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, na kutoa haki yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu makabila ya watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na ukombozi wangu hautakoma kamwe. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope masuto ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo atawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote. Amka, amka, jivike nguvu, Ee mkono wa Bwana; Amka kama katika siku zile za kale, Katika vizazi vile vya zamani. Si wewe uliyemkatakata Rahabu? Uliyemchoma yule joka? Si wewe uliyeikausha bahari, Na maji ya vilindi vikuu; Uliyevifanya vilindi kuwa njia, Ili wapite watu waliokombolewa? Nao waliokombolewa na BWANA watarejea, Watafika Sayuni, wakiimba; Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; Watapata shangwe na furaha; Huzuni na kuugua zitakimbia. Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani? Ukamsahau BWANA, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo ajitayarishapo kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye? Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma. BWANA wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.
Isaya 51:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta BWANA; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa. Mwangalieni Ibrahimu, baba yenu, na Sara, aliyewazaa; kwa maana alipokuwa mmoja tu nalimwita, nikambariki, nikamfanya kuwa wengi. Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya BWANA; furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba. Nisikilizeni mimi, enyi watu wangu; nisikieni, taifa langu; maana sheria itatoka kwangu, nami nitaistarehesha hukumu yangu iwe nuru ya mataifa. Haki yangu i karibu, wokovu wangu umekuwa wazi, na mikono yangu itawahukumu kabila za watu; visiwa vitaningoja, navyo vitautumainia mkono wangu. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao. Maana nondo itawala kama vazi, na funza atawala kama sufu; bali haki yangu itakuwa ya milele, na wokovu wangu hata vizazi vyote. Amka, amka, jivike nguvu, Ee mkono wa Bwana; Amka kama katika siku zile za kale, Katika vizazi vile vya zamani. Si wewe uliyemkata-kata Rahabu? Uliyemchoma yule joka? Si wewe uliyeikausha bahari, Na maji ya vilindi vikuu; Uliyevifanya vilindi kuwa njia, Ili wapite watu waliokombolewa? Nao waliokombolewa na BWANA watarejea, Watafika Sayuni, wakiimba; Furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; Watapata shangwe na furaha; Huzuni na kuugua zitakimbia. Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani? Ukamsahau BWANA, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye? Yeye aliyehamishwa na kufungwa atafunguliwa kwa haraka; wala hatakufa na kushuka shimoni, wala chakula chake hakitapunguka. Maana mimi ni BWANA, Mungu wako, niichafuaye bahari, mawimbi yake yakavuma. BWANA wa majeshi ndilo jina lake. Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.
Isaya 51:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki na mnaomtafuta BWANA: Tazameni mwamba ambako mlichongwa, na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa; mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, ambaye aliwazaa. Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu, nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi. Hakika BWANA ataifariji Sayuni, naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote; atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni, nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya BWANA. Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake, shukrani na sauti za kuimba. “Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Sheria itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa. Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama mainzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe. “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao. Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.” Amka, Amka! Jivike nguvu, ewe mkono wa BWANA, Amka, kama siku zilizopita, kama vile vizazi vya zamani. Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande, uliyemchoma yule joka? Si ni wewe uliyekausha bahari, maji ya kilindi kikuu, uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari ili waliokombolewa wapate kuvuka? Wale waliolipiwa fidia na BWANA watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao. Furaha na shangwe zitawapata, huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka. “Mimi, naam mimi, ndimi niwafarijie ninyi. Ninyi ni nani hata kuwaogopa wanadamu wanaokufa, wanadamu ambao ni majani tu, kwamba mnamsahau BWANA Muumba wenu, aliyezitanda mbingu na kuiweka misingi ya dunia, kwamba mnaishi katika hofu siku zote kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu, ambaye nia yake ni kuangamiza? Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu? Wafungwa waliojikunyata kwa hofu watawekwa huru karibuni; hawatafia kwenye gereza lao, wala hawatakosa chakula. Kwa maana Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume: BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake. Nimeweka maneno yangu kinywani mwako na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu: Mimi niliyeweka mbingu mahali pake, niliyeweka misingi ya dunia, niwaambiaye Sayuni, ‘Ninyi ni watu wangu.’ ”