Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 51:1-16

Isaya 51:1-16 NEN

“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki na mnaomtafuta BWANA: Tazameni mwamba ambako mlichongwa, na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa; mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, ambaye aliwazaa. Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu, nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi. Hakika BWANA ataifariji Sayuni, naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote; atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni, nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya BWANA. Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake, shukrani na sauti za kuimba. “Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Sheria itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa. Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini. Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama mainzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe. “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao. Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.” Amka, Amka! Jivike nguvu, ewe mkono wa BWANA, Amka, kama siku zilizopita, kama vile vizazi vya zamani. Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande, uliyemchoma yule joka? Si ni wewe uliyekausha bahari, maji ya kilindi kikuu, uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari ili waliokombolewa wapate kuvuka? Wale waliolipiwa fidia na BWANA watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao. Furaha na shangwe zitawapata, huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka. “Mimi, naam mimi, ndimi niwafarijie ninyi. Ninyi ni nani hata kuwaogopa wanadamu wanaokufa, wanadamu ambao ni majani tu, kwamba mnamsahau BWANA Muumba wenu, aliyezitanda mbingu na kuiweka misingi ya dunia, kwamba mnaishi katika hofu siku zote kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu, ambaye nia yake ni kuangamiza? Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu? Wafungwa waliojikunyata kwa hofu watawekwa huru karibuni; hawatafia kwenye gereza lao, wala hawatakosa chakula. Kwa maana Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume: BWANA Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake. Nimeweka maneno yangu kinywani mwako na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu: Mimi niliyeweka mbingu mahali pake, niliyeweka misingi ya dunia, niwaambiaye Sayuni, ‘Ninyi ni watu wangu.’ ”