Isaya 37:1-20
Isaya 37:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la BWANA. Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi. Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa. Yamkini BWANA, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo BWANA, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.” Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya, Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo. Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili kwamba atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ” Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna. Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia na neno hili: “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa? Yaani miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?” Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la BWANA, akaikunjua mbele za BWANA. Naye Hezekia akamwomba BWANA akisema: “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. Tega sikio, Ee BWANA, usikie; fungua macho yako, Ee BWANA, uone; sikiliza maneno yote ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai. “Ni kweli, Ee BWANA, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao. Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Sasa basi, Ee BWANA Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili kwamba falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee BWANA, ndiwe Mungu.”
Isaya 37:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mfalme Hezekia aliposikia habari hiyo alirarua mavazi yake, akavaa vazi la gunia, akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia. Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa, na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama anayetaka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa. Inawezekana kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya mkuu wa matowashi ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atapinga maneno aliyoyasikia; kwa hiyo waombee watu waliobaki.’” Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya, yeye akawaambia, “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Usiogope kwa sababu ya maneno ya watumishi wa mfalme wa Ashuru uliyoyasikia, maneno ambayo wameyasema kunidharau. Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi halafu atarudi katika nchi yake, na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’” Kisha yule mkuu wa matowashi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akishambulia mji wa Libna. Halafu aliposikia habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema, “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru. Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, unadhani wewe utaokoka? Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo wazee wangu waliyaangamiza? Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na Iva?’” Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema; “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, unayeketi katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Wewe ndiwe uliyeumba mbingu na dunia. Ee, Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka na kukutukana wewe Mungu uliye hai. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa yote na nchi zao. Waliweza kuitupa miungu yao motoni, kwa sababu haikuwa miungu kweli bali sanamu za miti au mawe zilizochongwa na mikono ya watu. Sasa ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utuokoe makuchani mwa Senakeribu, ili falme zote za dunia zijue kwamba wewe peke yako ndiwe uliye Mwenyezi-Mungu.”
Isaya 37:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wakiwa wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wako tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa. Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo kamanda ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia. Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya. Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia uvumi, na kurudi hadi nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe. Basi yule kamanda akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anapigana vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi. Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema, Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe? Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva? Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Hezekia akamwomba BWANA, akisema, Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe kutoka kwa mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.
Isaya 37:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa. Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia. Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya. Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe. Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi. Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema, Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe? Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva? Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Hezekia akamwomba BWANA, akisema, Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.