Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isa 37:1-20

Isa 37:1-20 SUV

Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA. Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa. Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia. Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya. Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe. Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi. Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema, Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe? Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva? Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Hezekia akamwomba BWANA, akisema, Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.

Soma Isa 37