Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 3:1-15

Isaya 3:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Sasa, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi ataondoa kutoka Yerusalemu na Yuda kila tegemeo: Tegemeo lote la chakula, na tegemeo lote la kinywaji. Ataondoa mashujaa na askari, waamuzi na manabii, waaguzi na wazee, majemadari wa vikosi vya watu hamsini, na watu wenye vyeo, washauri, wachawi stadi na walozi hodari. Mungu ataweka watoto wawatawale; naam, watoto wachanga watawatawala. Watu watadhulumiana, kila mtu na jirani yake; vijana watawadharau wazee wao, na watu duni watapuuza wakuu wao. Wakati huo ndugu atamwambia ndugu yake wakiwa bado nyumbani kwa baba yao: “Wewe unalo koti; utakuwa kiongozi wetu. Chukua hatamu juu ya uharibifu huu!” Lakini siku hiyo atasema, “Mimi siwezi kuwa mwuguzi, nyumbani mwangu hamna chakula wala mavazi. Msinifanye mimi kuwa kiongozi wenu.” Watu wa Yerusalemu wamejikwaa, watu wa Yuda wameanguka, kwa kuwa wanampinga Mwenyezi-Mungu kwa maneno na matendo, wakipuuza utukufu wake miongoni mwao. Ubaguzi wao unashuhudia dhidi yao; wanatangaza dhambi yao kama ya Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao watu hao, kwani wamejiletea maangamizi wenyewe. Waambieni waadilifu jinsi walivyo na bahati: Kwani watakula matunda ya matendo yao. Lakini ole wao watu waovu! Mambo yatawaendea vibaya, kwani waliyotenda yatawapata wao wenyewe. Watu wangu watadhulumiwa na watoto; wanawake ndio watakaowatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanavuruga njia mnayopaswa kufuata. Mwenyezi-Mungu yu tayari kuanza mashtaka, anasimama kuwahukumu watu wake. Mwenyezi-Mungu anawashtaki wazee na wakuu wa watu wake: “Nyinyi ndio mlioliharibu shamba la mizabibu; mali walizowanyanganywa maskini zimo nyumbani kwenu. Mnamaanisha nini kuwakandamiza watu wangu, kuwatendea ukatili watu maskini? Nauliza mimi Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi.”

Shirikisha
Soma Isaya 3

Isaya 3:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa maana, tazama, Bwana, BWANA wa majeshi, awaondolea Yerusalemu na Yuda egemeo na tegemeo; tegemeo lote la chakula na tegemeo lote la maji; mtu hodari na mtu wa vita; mwamuzi na nabii; mpiga ramli na mzee; jemadari aliye juu ya watu hamsini, na mtu mstahifu, na mshauri, na fundi aliye stadi, na mganga ajuaye uganga sana. Nami nitawapa watoto kuwamiliki, na watoto wachanga kuwatawala. Nao watu wataonewa, kila mtu na mwenziwe, na kila mtu na jirani yake; mtoto atajivuna mbele ya mzee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima. Mtu atakapomshika ndugu yake ndani ya nyumba ya baba yake, akisema, Wewe una nguo, ututawale wewe; na mahali hapa palipobomoka pawe chini ya mkono wako; basi, siku ile atainua sauti yake, akisema, Mimi sitakuwa mponya watu; kwa maana ndani ya nyumba yangu hamna chakula wala mavazi; wala hamtanifanya kuwa mtawala juu ya watu hawa. Kwa maana Yerusalemu umebomolewa na Yuda wameanguka, kwa sababu ulimi wao na matendo yao ni kinyume cha BWANA, hata wakayachukiza macho ya utukufu wake. Kuonekana kwa nyuso zao kwashuhudia juu yao, wafunua dhambi yao kama Sodoma, hawaifichi. Ole wa nafsi zao, kwa maana wamejilipa nafsi zao uovu. Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa malipo ya mikono yake. Kuhusu watu wangu, watoto ndio wanaowaonea, na wanawake ndio wanaowatawala. Enyi watu wangu, wakuongozao wakukosesha, waiharibu njia ya mapito yako. BWANA asimama ili atete, asimama ili awahukumu watu. BWANA ataingia katika kuwahukumu wazee wa watu wake na wakuu wao; Ninyi ndinyi mliokula shamba la mizabibu; vitu mlivyowateka maskini vi ndani ya nyumba zenu. Ni nini maana yake, ninyi kuwaonea watu wangu, na kuponda nyuso za maskini? Asema Bwana, BWANA wa majeshi.

Shirikisha
Soma Isaya 3

Isaya 3:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa maana, tazama, Bwana, BWANA wa majeshi, awaondolea Yerusalemu na Yuda egemeo na tegemeo; tegemeo lote la chakula na tegemeo lote la maji; mtu hodari na mtu wa vita; mwamuzi na nabii; mpiga ramli na mzee; jemadari aliye juu ya watu hamsini, na mtu mstahifu, na mshauri, na fundi aliye mstadi, na mganga ajuaye uganga sana. Nami nitawapa watoto kuwamiliki, na watoto wachanga kuwatawala. Nao watu wataonewa, kila mtu na mwenziwe, na kila mtu na jirani yake; mtoto atajivuna mbele ya mzee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima. Mtu atakapomshika ndugu yake ndani ya nyumba ya baba yake, akisema, Wewe una nguo, ututawale wewe; na mahali hapa palipobomoka pawe chini ya mkono wako; basi, siku ile atainua sauti yake, akisema, Mimi sitakuwa mponya watu; kwa maana ndani ya nyumba yangu hamna chakula wala mavazi; wala hamtanifanya kuwa mtawala juu ya watu hawa. Kwa maana Yerusalemu umebomolewa na Yuda wameanguka, kwa sababu ulimi wao na matendo yao ni kinyume cha BWANA, hata wayachukize macho ya utukufu wake. Kuonekana kwa nyuso zao kwashuhudia juu yao, wafunua dhambi yao kama Sodoma, hawaifichi. Ole wa nafsi zao, kwa maana wamejilipa nafsi zao uovu. Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa ijara ya mikono yake. Katika habari za watu wangu, watoto ndio wanaowaonea, na wanawake ndio wanaowatawala. Enyi watu wangu, wakuongozao wakukosesha, waiharibu njia ya mapito yako. BWANA asimama ili atete, asimama ili awahukumu watu. BWANA ataingia katika kuwahukumu wazee wa watu wake na wakuu wao; Ninyi ndinyi mliokula shamba la mizabibu; vitu mlivyowateka maskini vi ndani ya nyumba zenu. Ni nini maana yake, ninyi kuwaonea watu wangu, na kuseta nyuso za maskini? Asema Bwana, BWANA wa majeshi.

Shirikisha
Soma Isaya 3

Isaya 3:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Tazama sasa, Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda upatikanaji wa mahitaji na misaada, upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji, shujaa na mtu wa vita, mwamuzi na nabii, mwaguzi na mzee, jemadari wa kikosi cha watu hamsini na mtu mwenye cheo, mshauri, fundi stadi na mlozi mjanja. Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao, watoto ndio watakaowatawala. Watu wataoneana wao kwa wao: mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake. Kijana atainuka dhidi ya mzee, mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima. Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake katika nyumba ya baba yake na kusema, “Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu, tawala lundo hili la magofu!” Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema, “Sina uponyaji. Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu, msinifanye niwe kiongozi wa watu.” Yerusalemu inapepesuka, Yuda inaanguka; maneno yao na matendo yao ni kinyume na BWANA, wakiudharau uwepo wake uliotukuka. Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao, hujivunia dhambi yao kama Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao! Wamejiletea maafa juu yao wenyewe. Waambie wanyofu itakuwa heri kwao, kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao. Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao! Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda. Vijana wanawatesa watu wangu, wanawake wanawatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanawapoteza njia. BWANA anachukua nafasi yake mahakamani, anasimama kuhukumu watu. BWANA anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu. Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote.

Shirikisha
Soma Isaya 3