Isaya 3:1-15
Isaya 3:1-15 NEN
Tazama sasa, Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote, yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda upatikanaji wa mahitaji na misaada, upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji, shujaa na mtu wa vita, mwamuzi na nabii, mwaguzi na mzee, jemadari wa kikosi cha watu hamsini na mtu mwenye cheo, mshauri, fundi stadi na mlozi mjanja. Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao, watoto ndio watakaowatawala. Watu wataoneana wao kwa wao: mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake. Kijana atainuka dhidi ya mzee, mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima. Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake katika nyumba ya baba yake na kusema, “Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu, tawala lundo hili la magofu!” Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema, “Sina uponyaji. Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu, msinifanye niwe kiongozi wa watu.” Yerusalemu inapepesuka, Yuda inaanguka; maneno yao na matendo yao ni kinyume na BWANA, wakiudharau uwepo wake uliotukuka. Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao, hujivunia dhambi yao kama Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao! Wamejiletea maafa juu yao wenyewe. Waambie wanyofu itakuwa heri kwao, kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao. Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao! Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda. Vijana wanawatesa watu wangu, wanawake wanawatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanawapoteza njia. BWANA anachukua nafasi yake mahakamani, anasimama kuhukumu watu. BWANA anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu. Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote.