Isaya 24:1-23
Isaya 24:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa Mwenyezi-Mungu anaiharibu dunia na kuifanya tupu. Atausokota uso wa dunia na kuwatawanya wakazi wake. Kila mtu atapatwa na mambo yaleyale: Mtu wa kawaida na kuhani; mtumwa na bwana wake; mjakazi na bibi yake; mnunuzi na mwuzaji; mkopeshaji na mkopaji; mdai na mdaiwa. Dunia itaharibiwa kabisa na kuangamizwa; Mwenyezi-Mungu ametamka hayo. Dunia inakauka na kunyauka; ulimwengu unafadhaika na kunyauka; mbingu zinafadhaika pamoja na dunia. Watu wameitia najisi dunia maana wamezivunja sheria za Mungu, wamezikiuka kanuni zake, wamelivunja agano lake la milele. Kwa sababu hiyo laana inaitokomeza dunia, wakazi wake wanateseka kwa makosa yao. Wakazi wa dunia wamepungua, ni watu wachache tu waliosalia. Mizabibu inanyauka, divai inakosekana. Wote waliokuwa wenye furaha sasa wanasononeka kwa huzuni. Mdundo wa vigoma umekoma, nderemo na vifijo vimetoweka; midundo ya vinubi imekomeshwa. Hakuna tena kunywa divai na kuimba; mvinyo umekuwa mchungu kwa wanywaji. Mji uliohamwa umejaa uharibifu; kila nyumba imefungwa asiingie mtu. Kuna kilio barabarani kwa kukosa divai; shangwe yote imekoma, furaha imetoweka duniani. Mji ni magofu matupu; malango yake yamevunjwavunjwa. Kama vile zeituni chache tu juu ya mzeituni au tini chache tu juu ya mtini baada ya kumaliza mavuno, ndivyo itakavyokuwa katika nchi zote: Watu wachache watabakia hai. Watakaosalia watapaza sauti, wataimba kwa shangwe. Kutoka magharibi watatangaza ukuu wa Mwenyezi-Mungu, nao wakazi wa mashariki watamsifu. Watu wa mbali watalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tunasikia nyimbo za sifa kutoka miisho ya dunia, nyimbo za kumsifu Mungu aliye mwadilifu. Lakini mimi ninanyongonyea, naam, ninanyongonyea. Ole wangu mimi! Wasaliti wanaendelea kuwa wasaliti, usaliti wao unazidi kuwa mbaya zaidi. Hofu, mashimo na mitego, hivi ndivyo vinavyowangojeni enyi wakazi wa dunia. Atakayeikimbia hofu atatumbukia shimoni; atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni. Madirisha ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia inavunjikavunjika, inapasuka na kutikiswatikiswa. Inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda. Imelemewa na mzigo wa dhambi zake nayo itaanguka wala haitainuka tena. Siku ile Mwenyezi-Mungu ataliadhibu jeshi la angani kadhalika na wafalme wa duniani. Wote watakusanywa kama wafungwa shimoni; watafungwa gerezani pamoja kwa miaka mingi, na baada ya muda huo atawaadhibu. Kisha mwezi utaaibishwa, nalo jua litaona aibu kuangaza, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatawala huko Yerusalemu katika mlima Siyoni; ataonesha wazee wa watu wake utukufu wake.
Isaya 24:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tazama, BWANA ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake. Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida. Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana BWANA amenena neno hilo. Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu. Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua. Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma. Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao. Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote. Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka. Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu. Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, viko juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewalewa kama mlevi, nayo inawayawaya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena. Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi wataadhibiwa. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Isaya 24:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tazama, BWANA ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake. Na itakuwa kama ilivyo hali ya watu, ndivyo itakavyokuwa hali ya kuhani; kama ilivyo hali ya mtumwa, ndivyo itakavyokuwa hali ya bwana wake; kama ilivyo hali ya mjakazi, ndivyo itakavyokuwa hali ya bibi yake; kama ilivyo hali yake anunuaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake auzaye; kama ilivyo hali yake akopeshaye, ndivyo itakavyokuwa hali yake akopaye; kama ilivyo hali yake atwaaye faida, ndivyo itakavyokuwa hali yake ampaye faida. Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana BWANA amenena neno hilo. Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu. Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua. Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma. Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao. Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote. Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka. Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu. Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika. Dunia kuvunjika, inavunjika sana; dunia kupasuka, imepasuka sana; dunia kutikisika, imetikisika sana. Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela; na mzigo wa dhambi zake utailemea; nayo itaanguka, wala haitainuka tena. Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia; nao watakusanywa pamoja kama vile wakusanywavyo wafungwa katika shimo nao watafungwa katika gereza; na baada ya muda wa siku nyingi watajiliwa. Ndipo mwezi utatahayari, na jua litaona haya; kwa kuwa BWANA wa majeshi atatawala katika mlima wa Sayuni, na katika Yerusalemu, na mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Isaya 24:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tazama, BWANA ataifanya dunia kuwa ukiwa na kuiharibu, naye atauharibu uso wake na kutawanya wakaao ndani yake: ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai. Dunia itaharibiwa kabisa na kutekwa nyara kabisa. BWANA amesema neno hili. Dunia inakauka na kunyauka, dunia inanyongʼonyea na kunyauka, waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea. Dunia imetiwa unajisi na watu wake; wameacha kutii sheria, wamevunja amri na kuvunja agano la milele. Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia, watu wake lazima waichukue hatia yao. Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa, nao waliosalia ni wachache sana. Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka, watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni. Furaha ya matoazi imekoma, kelele za wenye furaha zimekoma, shangwe za kinubi zimenyamaza. Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake. Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa. Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia. Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande. Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa. Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa BWANA. Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni BWANA utukufu, liadhimisheni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!” Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani. Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa. Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena. Katika siku ile BWANA ataadhibu nguvu zilizoko mbinguni juu, na wafalme walioko duniani chini. Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani, watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi. Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana BWANA Mwenye Nguvu Zote atawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.